• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Jinsi ya kuandaa mandazi ya mdalasini

Jinsi ya kuandaa mandazi ya mdalasini

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 30

Muda wa mapishi: Dakika 30

Walaji: 5

Vinavyohitajika

  • unga wa ngano nusu kilo
  • sukari glasi ndogo nusu
  • chumvi kiasi robo kijiko cha chai
  • iliki punje 10
  • mdalasini kijiko 1 kidogo
  • custard kijiko kimoja cha chakula
  • samli kijiko 1
  • tui la nazi glasi ndogo 2
  • hamira vijiko 2
  • baking powder kijiko 1
  • mafuta ya kupikia nusu lita

Maelekezo

Chekecha unga kwa kutumia kichungi kwenye chombo utakachotumia kukanda unga wako.

Chukua kikombe weka hamira, sukari vijiko viwili, unga vijiko viwili na uache kwa dakika tano mpaka hamira ifure.

Chukua unga uliouweka kwenye chombo chako, weka baking powder, chumvi kiasi, sukari, hiliki na custard kisha changanya vizuri.

Chukua hamira iliyoumuka uichanganye na unga wako kisha weka tui lako kidogo kidogo na uanze kuukanda unga.

Kanda unga wako kwa dakika 10 mpaka uwe laini kisha uuache kwa muda wa dakika tano.

Ongeza samli na uendelee kuukanda unga kisha uweke kwenye bakuli na uufunike ili usipitishe hewa. Uache tena kwa muda wa dakika 10. Ukishaumuka, kata madonge na uyasukume kwa kutumia unga mkavu upate umbo la duara kubwa kama chapati hivi, ila lisiwe nene sana wala jembamba sana. Ni zamu sasa ya wewe kukata mandazi yako kwa umbo la pembe tatu ama jinsi upendavyo. Yaache mandazi yako yaumuke kwa dakika 10.

Mimina mafuta kwenye karai na uyaache yapate moto kiasi kisha anza kuweka vipande vyako; kipande kimoja baada ya kingine.

Hakikisha mandazi hayawi mengi kwenye karai ili yaachane na uweze kuyageuza kwa urahisi.

Andazi likiiva, epua na uweke kwenye chujio au shashi kulichuja mafuta ya ziada.

Furahia.

You can share this post!

Sergio Ramos apokea ofa kutoka Bayern Munich, PSG na...

Museveni ajitokeza hadharani baada uvumi kuhusu afya yake