• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
KIKOLEZO: Celebs na siasa 2022

KIKOLEZO: Celebs na siasa 2022

NA SINDA MATIKO

GHAFLA kama gesi ya soda ya Coca-Cola, tumeshuhudia idadi kubwa ya maceleb wakiibuka na kutangaza nia zao za kugombea nyadhifa mbalimbali za kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao Agosti 9.

Tayari wengi wame wameshajiuzulu nyadhifa za kazi walizokuwa wakitekeleza kwenye sekta mbali mbali ili kugombea.

Mwezi Januari, Polycarp Otieno wa Sauti Sol, na mdau mkubwa wa burudani Adelle Onyango waliwaza kwa sauti kuhusu mtindo unaoendelea wa maceleb kuchipuka kila leo na kutangaza azma zao.

Kwa maneno yao, wawili hao walikiri kuhofia ikiwa kama kweli maceleb waliotangaza nia ya kugombea, wana nia nzuri ya kuitumikia nchini au wameshawishika kufanya hivyo kutokana na tamaa zao wenyewe.

“Ni kama vile kila celeb katika nchi hii anagombea wadhifa fulani kwenye serikali mpya ijayo. Ninachojiuliza ni hili, je wadhifa wa kisiasa ndio taji la muhimu zaidi au kuna la ziada. Hivi kweli wana nia nzuri ya Wananchi? Nawaza tu,” aliandika Otieno.

“Sio mbaya wao kugombea, ila kinachonishangaza mimi ni kwamba hadi sasa hakuna hata mmoja wao aliyewasilisha manifesto yenye mipango kazi kuhusu wanavyonuia kuboresha tasnia ya burudani. Kila mtu kazi ni kusema tu, wanapania kuwasaidia vijana. Kivipi? alidakia Adelle.

Lakini si unajua tena, kila mwamba ngoma, lazima atavutia kwake. Walengwa hao, wametuhakikishia na kutusisitizia nia njema.

FRASHA – Mwakilishi Wadi Athi River

Kwa mara nyingine tena, mwanamuziki wa kundi la P-Unit Francis Amisi almaarufu Frasha atagombea kiti cha wadi ya Athi River baada ya kupoteza kwenye uchaguzi uliopita.

Frasha anasisitiza, anajitosa kwenye siasa kuwasakia ‘mavijanaa’ kazi.

“Vijana tunapaswa kujitosa kwenye siasa na uongozi tukiwa bado wachanga na wenye nguvu. Tumeona baadhi ya wenzetu walichofanya hasa kwa kupambania muziki wetu kwa mfano sheria ya haki miliki. Tusipogombea sasa tutabaki kuwalaumu wakongwe kwa kutotunyooshea mambo. Muhimu tuingia tujisukumie,” Frasha anasema.

JALANG’O – Ubunge Langa’ta

Kupitia kauliu mbiu ‘Utu na Watu’ mchekeshaji Jalang’o ameahidi kuwatumikia watu. Alianza kama mwigizaji, akawa mwigizaji, mtangazaji na sasa anasema anaamini kapata mwito wa kwenda kuwatumikia watu wa Lang’ata.

“Nilipojiunga na Chuo nilisomea shahada ya Community Development. Kimsingi masomo haya ni kumsaidia mtu kuwa na uelewa wa jamii na jinsi ya kuboresha maisha yao. Ndio sababu nimeingia kwenye safari hii,” Jalang’o anajitetea.

Baada ya kujiuzulu wadhifa wake pale Kiss FM, Jalang’o anasema hana Plan B, kama akifeli kushinda ubunge, basi atarejea kwenye maisha yake ya kawaida ya kuwa mshereheshaji.

RUFFTONE – Useneta Nairobi

Kwa zaidi ya miaka 20, Rufftone amekuwa akifanya muziki wa injili. Lakini sasa anasema atagombea useneta lengo lake kubwa ikiwa ni kuwapa vijana kazi.

Lakini kama wenzake, Rufftone ameshindwa kuweka wazi mipango kazi aliyonayo kufanikisha malengo hayo zaidi ya kupigia debe sera za naibu Rais William Ruto na chama chake cha UDA.

Kuhusu kwa nini alichagua chama cha UDA na wala sio cha ODM, Rufftone amekiri kwamba aliamua kumsapoti Ruto baada ya kutaka kulimana mapanga na mdogo wake kwenye uchaguzi uliopita kutokana na tofauti zao za kichama. Rufftone alifichua kuwa kwenye uchaguzi wa 2017 aligombana na Daddy Owen kwa sababu mdogo wake alisapoti ODM na yeye PNU. Kwa maneno yake, Rufftone hakuchagua chama kutokana na sera ila kutokana na tofauti za kifamilia.

MC JESSY- Imenti Kusini

Mshereheshaji na mchekeshaji Jasper Muthomi aliwashtua mashabiki wengi Septemba mwaka jana alipotangaza azma yake ya kuwa mbunge.

Toka kipindi hicho, amekuwa bize sana akijishughulisha na kampeni za eneo bunge la kwao. Jessy anasema aliamua kugombea baada ya kupewa baraka na wazee wa eneo bunge lake.

Jessy anasisitiza kuwa malengo yake ni kuleta mabadiliko ya kudumu Imenti.

“Wanaanchi wa Imenti wanataka mabadiliko, hilo wameliweka wazi kabisa. Wapinzani wangu wameahidi kufanya marekebisho. Hii ndio tofauti yangu na wao,” MC Jessy anasema.

NJAMBI KOIKAI – Dagoretti Kusini

Fyah Mummah hajamaliza hata mwaka toka aliporejea kwenye kazi yake ya utangazaji aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 10.

Ameshajiuzulu wadhifa wake na sasa anapiga kampeni. Ameahidi kuwapa vijana kazi, kuboresha sekta ya afya katika eneo bunge lake, kutatua tatizo la maji na pia kuwasaidia wakongwe.

Njambi Koikai. PICHA | MAKTABA

“Nimekuwa nikijihusisha na miradi mingi ya huduma kwa jamii katika eneo bunge langu. Ninayaelea vyema matatizo yetu na ningependa fursa ya kutatua baadhi ya ker hizo,” Koikai kaahidi.

ALEX MWAKIDEU – Ubunge Wundanyi

Baada ya miaka zaidi ya 15 kwenye utangazaji, Mwakideu naye kaamua kuwa mbunge. Kwa maneno yake, anasema anaitaka kuirejeshea jamii yake shukrani.

“Ninachotaka ni kuirudishia jamii mkono. Kule kwetu hamna maendelo ya maana yaliyofanywa kwa miaka mingi. Ni wakati nikaweka hayo sawa,”

ANITA SOINA – Ubunge Kajiando Kaskazini

Mwanamazingira Anita anasema anarudi kijijini kutatua kero za eneo bunge lake kwa sababu anazielewa vizuri.

Anita Soina. PICHA | MAKTABA

“Nimezaliwa na kulelewa kule. Nimekuwa mwanaharakati wa kimazingira lakini sasa nataka niwapiganie watu wangu. Kule nitokako nazielewa kero zetu sababu nimekulia kule na nafikiri hatua ya kwanza ya kutatua tatizo ni kuwa kwenye nafasi ya kutoa suluhisho,” anasema.

You can share this post!

Ruto apaka Uhuru tope Amerika

Polisi bandia ashtakiwa kuteka nyara wanahabari wawili...

T L