• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
KIKOLEZO: Wameamua kukaa ngumu!

KIKOLEZO: Wameamua kukaa ngumu!

Na THOMAS MATIKO

KWA kawaida huwa tunawaonea gere watoto wa mastaa waliofanikiwa au wanaotoka kwenye familia za kitajiri.

Kwa mfano Anerlisa Muigai alipoingia kwenye mahusiano na mwanamuziki Ben Pol, wapo wengi waliodai kuwa jamaa amekwenda kumkamua pesa.

Ben Pol mwenyewe aliwahi kukiri jinsi wanamuziki kibao walivyokuwa wakijaribu kumtongoza Anerlisa baada yake kuanzisha mahusiano naye.

Ni uhusiano ulioonewa gere na wengi. Na hata sasa baada yao kuachana, Anerlisa hakosi kukashifiwa kwa sababu wengi wanaumwa na yale maisha ya kifahari anayoishi. Nina uhakika tabaka hili linaumia kichwa hata zaidi kwa kufahamu kuwa ndiye atakayerithi mali za mabilioni ya pesa zilizotengenezwa na wazazi wake.

Lakini sio wazazi wote mastaa wenye mipango kama hiyo ya kuwarithisha watoto wao mali yao, kama jinsi bilionea Chris Kirubi alivyofanya.

ELTON JOHN

UTAJIRI: Sh56 bilioni

Nguli huyu wa muziki wa Pop ambaye ni raia wa Uingereza alifunga ndoa na ‘mume’ wake David Furnish, 2005.

Kwa pamoja wana watoto wawili wa kiume waliowapata kupitia njia ya kuchukua mimba (surrogacy).

Mwanamuziki Elton John. Picha/ Hisani

Akiwa na umri wa miaka 74, na watoto wachanga ambao hata bado hawajafikia umri wa kubalehe, Elton hana mpango wa kuwaachia urathi wowote.

Kulingana naye, watoto hawapaswi kudekezwa hasa na mali ya wazazi kwa sababu huko ni kuharibu maisha yao.

Yeye na Furnish wameamua kutowaachia urithi watoto wao wawili. Miaka mitatu iliyopita walitoa Sh8 bilioni kama msaada wakisisitiza walifanya hivyo ili iwe funzo kwa wana wao kuhusu umuhimu wa kuheshimu njia za kupata riziki na pesa.

JACKIE CHAN

UTAJIRI: Sh38 bilioni

Kufikia 2015, jarida la Forbes lilikadiria utajiri wa mwigizaji huyu mkongwe kuwa bilioni 38. Ni dhahiri kuwa kiwango hicho kitakuwa kimeongezeka pakubwa kufikia sasa.

Akiwa na umri wa miaka 67, bado anatajwa kuwa mwigizaji anayelipwa vizuri Barani Asia.

Mwigizaji Jackie Chan ambaye jina lake halisi ni Fang Shilong. Picha/ Hisani

Ana watoto wawili na alishatangaza kuwa hana nia ya kuwaachia wanawe chochote. Badala yake atatoa mali yake kwa mashirika ya kuwasapoti watu wasiojiweza.

Ni uamuzi ambao ulimshangaza binti yake ambaye hawana ukaribu kama ilivyo na mwanawe wa kiume. Chan anasema kwamba, anaamini watoto wake wana maarifa ya kujichumia riziki na kama hawana basi kuwaachia mali yake itakuwa kazi bure sababu wataitumia vibaya wakati yeye alihangaika kuipata.

MARK ZUCKERBERG

UTAJIRI: SH14 Trilioni

Mwasisi na mumiliki wa mitandao ya kijamii Facebook na Instagram, yupo kwenye listi ya watu tano bora matajiri zaidi duniani.

Pamoja na mkewe Priscilla Chan wamejaliwa watoto wawili. Lakini kwenye wosia wao, hawana mpango wa kuwaachia wana wao hata sumuni.

Mwasisi wa Facebook Mark Zuckerberg akiwa jijini Washington, DC, Amerika, Oktoba 23, 2019. Picha/ AFP

Utajiri wao wote utaenda kwa wakfu wa Zuckerberg.

Fedha hizo zitatumika kusaidia katika uboreshaji wa sekta za afya, masomo na maisha ya watu wasiojiweza.

ASHTON KUTCHER & MILA KUNIS

UTAJIRI: SH11 Bilioni

Waigizaji hawa walifunga ndoa 2015. Kwa pamoja wamejaliwa watoto wawili. Licha ya mafanikio yao makubwa, nao vilevile hawana mpango wa kuwaachia chochote wanao.

Ashton Kutcher na Mila Kunis. Picha/ Hisani

Kulingana nao, suala la kuwarithisha watoto wao mali yao, ni kuwafanya wazembe na kuwanyima nafasi ya kuonyesha uwezo wao wa kujitengenezea rikizi. Kwa sababu hiyo, wamefanya uamuzi wa kuachia mashirika ya kuwasaidia watu wasiojiweza mali yao.

Hata hivyo Ashton anasema hatasita kumsapoti mtoto wake ikiwa ataibuka na mbinu kazi ya kujichumia rikizi.

GEORGE LUCAS

UTAJIRI: SH580 Bilioni

Ni mtayarishi wa filamu aliyeibuka na msururu wa filamu za Star Wars na vile vile Indiana Jones.

Utajiri wake uliongezeka maradufu baada ya kuiuzIa hakimiliki ya Star Wars pamoja na kampuni yake LucasFilm kampuni ya The Walt Disney.

Baba huyo wa watoto wanne naye hana mpango wa kumwachia mtoto wake yeyote mali yake. Mrithi wa mali yake ni wakfu wa George Lucas Educational Foundation, unaojihusisha na utafiti na jinsi ya kuboresha. Pia unatoa msaada wa elimu kwa familia zisijoziweza.

TANBIHI: Hawa tu ni baadhi ya mastaa wenye mawazo sawia kuhusiana na utajiri wao. Wengine ni kama vile Bills Gates, Michael Bloomberg, Warren Buffet miongoni mwa wengine.

You can share this post!

Ruto avuliwa GSU

Okutoyi apigwa breki nusu-fainali ya tenisi ya kimataifa ya...