• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Okutoyi apigwa breki nusu-fainali ya tenisi ya kimataifa ya J3 jijini Cairo

Okutoyi apigwa breki nusu-fainali ya tenisi ya kimataifa ya J3 jijini Cairo

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Angella Okutoyi amesimamishwa katika nusu-fainali ya mashindano ya tenisi ya daraja la tatu (J3) baada ya kulemewa na raia wa Brazil Ana Candiotto kwa seti 2-1 jijini Cairo nchini Misri hapo Agosti 26.

Okutoyi alianza vibaya mchuano huo akipoteza seti ya kwanza kwa alama 6-4. Alijikakamua na kutwaa seti ya pili kwa alama 6-1, lakini akanyamazishwa katika seti ya mwisho 6-2.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 17 alikuwa amebandua Wamisri Maria Charl na Jermine Sherif kwa seti 2-0 katika raundi mbili za kwanza na kupepeta raia wa Romania Briana Szabo 2-1 katika robo-fainali.

Candiotto alipiga Mrusi Violetta Borodina 2-0, Karina Jumazhanova (Kazakhstan) 2-1 na Daria Yesypchuk (Ukraine) 2-1 katika usanjari huo kabla ya kuzima Okutoyi.

Okutoyi na Candiotto,17, wanaorodheshwa katika nafasi ya 196 na 188 katika viwango bora chipukizi vya Shirikisho la Tenisi Duniani (ITF), mtawalia. Candiotto atakabiliana na Mmoroko Aya El Aouni (152 duniani) katika fainali Agosti 27. Aouni alibandua Sofia Nagornaia (Urusi), Sanjana Sirimalla (India), Yasmin Ezza (Misri) na Roisin Gilheany (Australia) kwa kuwanyuka seti 2-0 kila mmoja.

You can share this post!

KIKOLEZO: Wameamua kukaa ngumu!

Kane abeba Spurs hadi hatua ya makundi ya Europa Conference...