• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:59 AM
MALEZI KIDIJITALI: Kuepushia mtoto wako kutekwa na ponografia

MALEZI KIDIJITALI: Kuepushia mtoto wako kutekwa na ponografia

UKITAKA mtoto wako asitekwe na kupotoshwa na ponografia kwenye mtandao ni lazima uwe na ujasiri wa kumweleza wazi hatari za picha na video hizo chafu.

Utafiti uliofanywa nchini Australia, New Zealand na Uingereza unaonyesha kuwa wazazi wanaochukua hatua ya ujasiri na kuzungumza na watoto wao kuhusu hatari za ponografia na masuala ya ngono kwa jumla huwa wanawatendea haki.

“Wazazi walio na ujasiri wa kuketi na watoto wao kuzungumzia hatari ya ponografia huwa wanawasaidia watoto wao wasitekwe, kushirikishwa katika biashara hii chafu na kupotoshwa na tabia na uraibu huo,” unasema utafiti wa mashirika ya Esafety na Netsafe.

Wataalamu waliofanya utafiti huo wanasema kuwa mzazi anapozungumza na mtoto wake mapema na kujibu maswali anayomuuliza kuhusu hatari za ponografia, huwa anamuandaa mapema kukabiliana na hatari ikijiri.

Watafiti walisema kwamba wazazi saba kati ya kumi huwa hawajui wanachofaa kujibu wakiulizwa lolote kuhusu ponografia na watoto wao. Hii inaonyesha kuwa wazazi wanaweza kuwa chanzo cha watoto kuingia katika hatari inayotokana na uraibu wa kutazama au kushirikishwa katika biashara hii.

“Kuna haja ya wazazi hasa katika jamii za Kiafrika kutupilia mbali dhana kwamba kuzungumzia watoto masuala ya ngono ni mwiko. Huu ni ulimwengu wa dijitali ambayo imefuta kilichochukuliwa kuwa mwiko,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Ian Doras.

Anasema kwamba mzazi wa Kiafrika anapaswa kuwa msitari wa mbele kuzungumzia hatari za ponografia na watoto wake kwa sababu ndio wanaolengwa sana na wanaofanya biashara hiyo mtandaoni.

“Watoto wa Kiafrika wananyemelewa na wanaofanya biashara hii kwa kuwa hawafahamu jinsi ya kujilinda na hivyo basi wanaweza kupotoshwa kwa urahisi na athari zake ni hasi kwao binafsi, wazazi wao na jamii. Hivyo basi, mzazi anafaa kuwajibika mapema kuokoa mtoto wake na wanaowawinda mtandaoni,” asema Doras.

  • Tags

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Uhusiano ukidorora, hisia nazo huyoyoma

MAPISHI KIKWETU: Biriani ya Uyoga

T L