• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Mradi wa serikali wa kurembesha jiji wageuzwa eneo la kutupa taka

Mradi wa serikali wa kurembesha jiji wageuzwa eneo la kutupa taka

Na SAMMY KIMATU

[email protected]

MRADI mmoja wa kurembesha jiji la Nairobi ulioko katika eneo la Viwanda la Nairobi ambao uligharimu mlipa ushuru mamilioni ya pesa, umegeuzwa kuwa eneo la kutupa taka.

Hali ya mradi uliopo kati ya mzunguko wa barabara za Jogoo na Lusaka kuelekea mzunguko wa barabara kuu ya Mombasa na makutano ya barabara kuu ya Uhuru kupitia barabara ya Lusaka, ni ya kusikitisha.

Rundo la taka limewekwa karibu na uwanja wa City kwenye mzunguko wa barabara ya Jogoo.

Pia kuna uvundo katika eneo lililo mkabala wa barabra ya Lusaka karibu na lango kuu la kampuni ya Saghani.

“Rundo la taka linaonekana karibu na lango kuu la Saghani Garage wakati waendeshaji bod boda wamejenga kibanda cha kujikinga jua kali na mvua kwenye mradi huo. Sehemu nyingine iliyotumika kutupia taka iko karibu na bomba la maji mkabala na kituo cha mafuta cha Ola,” mwanamke mmoja anayechuuza chakula kando ya barabara ya Lusaka alisema.

Wakati wa mchana, wafanyakazi ndani ya eneo la Viwanda na vijana wa kurandaranda barabarani hutumia eneo hilo kama bustani wakilala pale kupumzika.

Isitoshe, mara nyingi, matatu hutumia eneo lililokuwa limepambwa kwa maua mara moja ili kuepuka msongamano wa magari.

Zaidi ya hayo, waendeshaji bodaboda wamebuni njia ndani ya mradi wenyewe.

Sehemu ya mradi wa urembeshaji wa jiji la Nairobi uliotiwa doa kando ya barabara ya Lusaka eneo la Viwanda, Nairobi, Septemba 16, 2020. Kando na rundo la taka, vijana wa kurandaranda wamegeuza mradi huo pahala pa kutulia. Mradi huo uliokuwa chini ya Mike Sonko ulihamishiwa NMS. Picha/ Sammy Kimatu

Mradi huo ulianzishwa na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko.

Baadaye, mradi huo ulitolewa chini ya usimamizi wa serikali ya Kaunti ya Nairobi na kuwa chini ya idara ya Utoaji Huduma za Jiji la Nairobi (NMS).

Mradi huo uliunda ajira kwa mamia ya vijana Nairobi.

Kadhalika, mradi huo ulipendeza macho kwa kuwa kulikuwa na nyasi iliyopandwa na kukatwa vizuri, maua mbalimbali yenye rangi za kuvutia na miti ilikuwa pia imepandwa.

Wakati huu, miti imekatwa, ua uliokuwepo haupo baada ya wahalifu kuiba nyaya na vikingi vilivyotumiwa kupitisha nyaya vikianguka baada ya kugongwa na magarai na pikipiki.

“Hatimaye, vikingi vya stima navyo havijasazwa kwani madereva walevi wameshuhudiwa wakivigonga na kuharibu taa za barabara,” mlinzi wa usiku katika kampuni moja karibu na mradi huo akaambia Taifa Jumapili.

You can share this post!

DINI: Siku njema huonekana asubuhi, ijaze dua na...

Gharama ya maisha kupanda kufuatia ongezeko la bei ya mafuta