• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Nitaongezaje mafuta mwilini?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nitaongezaje mafuta mwilini?

Mpendwa Daktari,

Kwa miezi kadhaa sasa uzani wangu umekuwa kati ya kilo 68 na 70 na kimo changu ni sentimta 180. Nina hamu kubwa ya chakula na hata nimekuwa nikitumia vijalizo vya vyakula (supplement foods). Nimefanyiwa chunguzi kadha kubaini iwapo nina maradhi yoyote lakini zote zinaonyesha kwamba sina tatizo. Nina wasiwasi. Nifanye nini kuongeza mafuta mwilini?

Erikah, Mombasa

Mpendwa Erikah,

Kimo cha sentimita 180 na uzani wa kati ya kilo 68 na 70 yaonyesha kwamba una afya. Kimo chako kikilinganishwa na uzani wako (BMI) ni 21 (BMI ya kawaida ni kati ya 18 na 25).

Japo kuna baadhi ya watu wanaoongeza uzani upesi, wengine hawabadilishi uzani kwa urahisi. Ni afya nzuri kuwa na uzani usiobadilika sana.

Unapozidi kukomaa kiumri, itakuwa rahisi kuongeza uzani kwani mfumo wa umetaboli utakuwa chini. Dhana kwamba unene ni ishara ya afya njema ni potovu.

Ikiwa uzani wako ni thabiti na uko katika kiwango sawa cha afya, na haukumbwi na matatizo ya kiafya kama vile kushambuliwa na maradhi upesi, basi haupaswi kua na wasiwasi.

Zingatia lishe yenye afya, fanya mazoezi na ujiepushe na tabia zinazokuweka kwenye hatari kiafya, kama vile kuvuta sigara au kunywa pombe kupindukia. Unapaswa kuukubali mwili wako jinsi ulivyo kwani uko sawa.

Mpendwa Daktari,

Nina tatizo na mba. Nimejaribu aina nyingi za mafuta bila mafanikio. Je kuna suluhisho kwa hili tatizo?

Jane, Mombasa

Mpendwa Jane,

Mba ambazo pia zinafahamika kama seborrheic dermatitis, ni tatizo la ngozi linalosababisha mwasho na chembechembe za magamba.

Kwa kawaida huathiri ngozi ya kichwa, lakini pia zaweza athiri sehemu nyingine za mwili. Kiini chake hakijulikani, lakini pia zaweza tokana na mawazo mengi, ngozi yenye mafuta mengi, au maambukizi ya kuvu, vile vile baridi. Kuna baadhi ya matatizo ya kiafya na dawa ambazo pia zaweza chochea shida hii. Mambo huwa mabaya na kuimarika baada ya muda.

Unaweza tumia shampuu au krimu kama vile ketoconazole selenium, zinc au salycilic acid. Kwa kawaida dawa hizi zinauzwa katika maduka ya dawa au zaweza pendekezwa na daktari.

Pia, kunywa maji mengi na udumishe lishe bora. Pia, jaribu usijikune kichwani kwani hii yaweza sababisha maambukizi. Iwapo tatizo hili litandelea licha ya kutumia dawa hizi, tafuta ushauri kutoka kwa mtaaalamu wa ngozi (dermatologist).

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Nimonia: Nduli anayewaandama watoto kila...

Hazard na De Bruyne kukosa gozi kali la robo-fainali ya...