• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Uvimbe kwenye titi na chuchu

PATA USHAURI WA DKT FLO: Uvimbe kwenye titi na chuchu

Mpendwa Daktari,

Nini kinachosababisha uvimbe wa titi na chuchu (breast and nipple thrush).

Jaylene, Mombasa

Mpendwa Jaylene,

Uvimbe huu hutokana na maambukizi ya ukuvu kwa jina Candida albicans ambao waweza tokea kwenye chuchu au tishu za titi, na hata katika sehemu zingine mwilini.

Ikiwa una uchungu kwenye chuchu ambao hauishi, basi unapaswa kuzungumza na daktari kwani iwapo hali hii itagunduliwa mapema itakusaidia unaponyonyesha.

Uvimbe wa aina hii unaweza husishwa na maambukizi ya vaginal thrush, matumizi ya kiua vijasumu au jeraha kwenye chuchu.

Dalili ya kwanza ni maumivu kwenye chuchu, titi au sehemu hizi zote. Uchungu huwa mwingi sana kiasi cha kusababisha maumivu makali hata unapovalia nguo. Hasa uchungu huu hushuhudiwa pindi baada ya kunyonyesha.

Huenda chuchu zako zikabadili rangi na kuonekana pinki huku sehemu nyeusi ikibadilika rangi na kuwa nyekundu, kukauka na kunyakuka. Aidha chuchu hupata na jeraha na kuchubuka na kwa mara nyingi huchukua muda kabla ya kupona.

Pia ishara za uvimbe zaweza jitokeza mdomoni na kwenye tako la mtoto au sehemu hizi zote. Mdomoni, uvimbe huu utaonekana kama safu nyeupe kwenye ulimi au madoa meupe katika sehemu ya ndani ya mashavu au sehemu hizi zote. Kwenye tako, ishara itajitokeza mfano wa upele mwekundu ulio na madoa, hali ambayo haiishi hata baada ya kupaka krimu za kupambana na ukuvu.

Uvimbe huu hutibiwa na dawa za kupambana na ukuvu, huku ukihitajika kutibu uvimbe mwingine wowote unaowakabili jamaa zako. Hakikisha kuwa chuchu zako zinasalia kavu kwani uvimbe kwenye titi hutokea katika sehemu zenye unyevu na joto.

Ili kuzuia hali hii isisambae, nawa mikono kwa sabuni na maji safi pindi baada ya kumbadilisha mtoto nepi na kabla ya kujipaka mafuta. Safisha taulo na sidiria katika maji moto ya sabuni na uanike kwenye jua.

Mpendwa Daktari,

‘Paronychia’ ni maradhi yapi?

Elvis, Nairobi

Mpendwa Elvis,

Ni hali ambayo huanza kwa uvimbe mwekundu kwenye kucha. Kwa kawaida husababisha maumivu makali huku sehemu iliyoathitika ikibadili rangi na kuwa kijani au manjano.

Ishara za tatizo hili ni pamoja na uvimbe, mkusanyiko wa usaha, sehemu iliyoathirika kuwa nyekundu na maumivu unapogusa sehemu hiyo.

Pata ushauri wa daktari ikiwa rangi nyekundu itaenea katika sehemu zingine mbali na eneo linalozunguka kucha. Rangi hii inaashiria kuwa shida hii ni zaidi ya maambukizi ya kucha. Nenda hospitalini usaha unapojikusanya kwani utamhitaji daktari kuuondoa.

Hali hii husababishwa na jeraha kwenye kucha, ukaya wa kucha ambao waweza sababisha maambukizi madogo na hivyo kufanya ngozi inayozunguka kucha kuwa nyepesi.

Pia kuuma kucha husababisha maumivu kwa kaya zinazovuja. Kadhalika tabia hii huongeza uwezekano wa maambukizi ya bakteria kwenye kucha na mdomoni mwako.

Ili kuzuia hali hii kutokea, unashauriwa usiume kucha; valia glavu za mpira unapojihusisha katika shughuli zinazohusisha matumizi mengi ya maji; dhibiti maradhi ya kudumu kama vile kisukari na pia nawa mikono kila mara hasa ikiwa kazi yako inahusisha kugusa uchafu kama vile useremala, au kazi yoyote ambapo mikono yako inachafuka na kukumbwa na majeraha.

You can share this post!

Raila akausha marafiki

SHINA LA UHAI: Jinsi mihadarati inavyoua vijana kwa maradhi...