• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
USANII MASHINANI: Msanii na mtangazaji wa runinga, studio mtandaoni

USANII MASHINANI: Msanii na mtangazaji wa runinga, studio mtandaoni

Na PATRICK KILAVUKA

STEPHEN Macharia ni msanii ambaye amejiinua kutoka mavumbini hadi kustawisha studio na kituo cha runinga mtandaoni.

Kwao Nyandarua watu wengi wanamtambua kama mwimbaji wa nyimbo za Injili za kizazi kipya.

Hata hivyo, akiwa bado mchanga alitamani sana kuwa msanii na mtangazaji.

Safari hii aliianza kwa kuimba katika krusedi na mikutano mingine ya Injili.

Sasa amefikia upeo wa kumiliki kituo cha runinga mtandaoni chenye anwani ya Hill Star TV; kinapatikana kupitia mtandao wa www.hillstartv.co.ke au mtandao wa kijamii wa Facebook: hillstartvkenya.

Matunda hayo ni zao la zaidi ya mwongo mmoja katika majukwaa ya nyimbo za Injili.

Kisha akatumia talanta yake kujifungulia milango ya kuwa mtangazaji kwenye vituo kadhaa, ambapo alizoa maarifa yaliyomwezesha kufungua kituo chake.

Macharia ni mzaliwa wa Kangui katika Kaunti ya Nyandarua. Alisomea Shule ya Msingi ya Kangui kabla kujiunga na sekondari ya Nyandarua Boys.

Ari yake ya uimbaji ilichipuza akiwa darasa la saba. Wakati huo, alighani wimbo Mwokozi uliotikisa ulingo wa muziki wa Injili na kuuchomoa akiwa kidato cha tatu.

Ulikuwa ushuhuda wake wa kumrudishia Maulana shukrani baada ya kumponya. Baada ya masomo alipata kibarua kwa mjomba wake mjini Kajiado kuuza magazeti. Ujira wake aliuweka akiba akautumia kama mtaji wa kurekodi nyimbo zake.

Akaingia studio ya Mopotunes na kuchomoa kibao Anaweza – ujumbe ambao anasema aliupata akifanya kazi.

Baada ya wimbo huo alipata fursa ya kuhudumu katika kanisa la House of Mercy Prophetic Ministry chini ya Kasisi Sammy Lukwaro; akiwa na wasanii wengine David Kipkiteri na mwingine anayemkumbuka tu kwa jina Omondi.

Walijulishwa kwa mmiliki wa studio ya Afro Studio, Musa Mwangi, aliyewapokea kwa moyo mkungufu na hata kuwawezesha kurekodi albumu ya “Tumefika”.

Nyimbo zake zinamuingizia kima cha Sh50,000 kupitia mauzo ya mtandaoni.

Katika hazina yake ya nyimbo Macharia ana santuri tatu; ambazo ni nyimbo alizitunga akiwa shuleni na zikapata mashiko.

Anakumbuka siku aliyekuwa Mama wa Taifa, mwendazake Lucy Kibaki, alitembelea shule yao ya upili na kijana huyu akapata fursa ya kupeperusha wimbo wake “Kila Kiumbe Kimsifu Bwana”, uliowagusa waheshimiwa waliokuwepo.

Macharia ana albamu kadhaa kufikia sasa: Namshukuru, Muthamaki na ya tatu ya wimbo Moyo Wangu. Alianza kunengua akiwa darasa la saba na talanta hiyo ilimpa fursa ya kusakata muziki kwenye majukwaa ya krusedi, kanisani na mialiko.

Akaunda kikundi cha Unitaz Dance Crew ambao huwasakatia waimbaji wakati wa kurekodi kanda za video, kwa ada ya Sh1,500.

Kutangamana na wasanii na watangazaji kulimpa jukwaa la kujitanua zaidi akapata fursa ya kushiriki vipindi kwenye vituo mbalimbali, kabla kuajiriwa na runinga ya Miracles Television Network, Kenya (MTV Kenya).

Hapo alipata uzoefu wa kuendesha programu ya Kigocho Interview Show akishirikiana na mtangazaji Jacky Muthoni ambaye kwa sasa yuko Maajabu TV.

Kipindi hiki alichohudumu katika stesheni hizo kilimfunza mambo mengi ya kuendesha studio na runinga; akapata tajriba ambayo ilimfaa sana alipofungua runinga yake ya Hillstartv mtandaoni.

Runinga hiyo inahusishwa na ukuzaji wa wasanii, uelimishaji, uhamasishaji na utumbuizaji; mbali na kurekodia wasanii muziki studioni.

Hata hivyo, yeye bado ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo.

Changamoto kuu ilikuwa mtaji wa kusajili mtandao wake wa televisheni na pesa za kununua vifaa vya studio.

Mapato yake anazoa kwa kuwaunganishia wateja mawimbi ya runinga hiyo mtandaoni kwa ada ya Sh10,000; ambapo hupata wasiopungua watano kila mwezi.

You can share this post!

KILIMO BIASHARA: Msomi wa biashara aliyezamia zaraa ya...

Adai kortini akivuta bangi huongeza nguvu za kiume