• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
WANDERI KAMAU: Ughaibuni si mbinguni, huko pia kuna magumu

WANDERI KAMAU: Ughaibuni si mbinguni, huko pia kuna magumu

Na WANDERI KAMAU

DHANA kuu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu katika nchi zenye chumi za kadri ni kuwa, maisha katika mataifa yaliyostawi kiuchumi huwa bora.

Ni taswira aliyochora marehemu Prof Ken Walibora, kwenye novela ‘Ndoto ya Amerika’, inayorejelea ndoto ya kijana mmoja aliyetamani sana kwenda Amerika ili kutimiza ndoto zake maishani.

Ingawa malengo yake hayakutimia kama alivyotarajia, simulizi kuu iliyo kwenye novela hiyo ni picha halisi iliyo katika vijiji tunakotoka.Wale waliofanikiwa kusafiri na kukaa ughaibuni huonekana kama ‘miungu wadogo.’

Huwa wanachukuliwa kama watu waliopiga hatua kubwa maishani, kiasi kwamba kila mmoja anayewazunguka hutamani kusafiri ng’ambo “kuchuma mazuri yaliyo huko”.

Imani hiyo imejenga dhana mbaya miongoni mwa vijana katika mataifa hayo, kiasi kuwa wengi wao wamepoteza kabisa uzalendo kuhusu nchi zao.

Kwa sasa, kila kijana anatamani kusafiri ughaibuni kutokana na hali ngumu ya maisha iliyo katika nchi nyingi zenye chumi za kadri, hasa barani Afrika.

Hata hivyo, kile ambacho wengi wanasahau ni kuwa, kinyume na dhana hizo, maisha ya ughaibuni si rahisi kama ambavyo imekuwa ikielezwa kupitia majukwaa mbalimbali.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya raia kutoka nchi hizo wanaosafiri Ulaya imeongezeka sana, ambapo hilo limegeuka kuwa janga kuu linaloyakabili mataifa hayo.

Mataifa kama Italia yamependekeza sheria kali ili kudhibiti idadi ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini humo kutoka Afrika na kwingineko duniani, hasa kupitia Ziwa Mediterranean.

Kila mwaka, imekuwa kawaida kwa ripoti kuibuka kuhusu mamia ya Waafrika wanaofariki katika ziwa hilo wakitumia njia za mkato kujaribu kuingia Ulaya kujiendeleza kimaisha.

Hapa Kenya, si jambo la kusikitisha tena kuhusu idadi kubwa ya Wakenya wanaotesekea katika nchi za Arabuni mikononi mwa waajiri wakatili.

Wengi wanaojipata kwenye masaibu hayo ni mabinti wachanga wanaoenda katika nchi hizo kutafuta kazi za kuwa vijakazi katika makazi ya watu matajiri.

Katika mataifa kama Amerika na Ujerumani, watu wengi wamekuwa wakilalamikia kubaguliwa kwa misingi ya rangi zao.Ni katika nchi hizo ambapo visa vya watu kuuana kwa kufyatuliana risasi huwa vinaripotiwa mara kwa mara. Wakenya wamejipata kuwa waathiriwa wa maovu hayo.

Kutokana na uhalisia huo, imefika wakati kwa vijana katika mataifa hayo kuzinduka na kufahamu kuwa maisha ya ughaibuni si “mbinguni” kama wengi wanavyoamini.Si rahisi, bali yanaandamwa na mahangaiko ya kawaida kama ilivyo katika nchi zao.

Hata hivyo, ubora uliopo katika nchi nyingi ni kwamba nyingi huwa na mifumo bora ya kiutawala, inayodhibiti sekta muhimu kama elimu, afya na masuala ya ajira.Hata hivyo, hilo halimaanishi wenyeji huwa hawafanyi kazi.

La. Wao hujituma kama kawaida ili kupata riziki zao.Hivyo, badala ya kuendelea kuhamia ughabuni “kutafuta mazuri’ yasiyokuwepo, ni wajibu wao kuamka na kuzishinikiza serikali katika nchi zao kuboresha mifumo ya uongozi na usimamizi wa sekta muhimu.

Ni kupitia hilo pekee watakapochangia uboreshaji wa nchi zao, badala ya kuendelea kuhamia ughaibuni bila kufanikiwa kutimiza ndoto zao.

[email protected]

You can share this post!

Historia ya Malindi kama mji wa kifahari Uswahilini

Sheria ya watu fisadi kuepuka korti yatua bungeni