• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
WASONGA: Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki afutwe kwa utepetevu

WASONGA: Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki afutwe kwa utepetevu

Na CHARLES WASONGA

AFISI ya Mwanasheria Mkuu ni muhimu zaidi katika utendakazi wa serikali ya Kenya kwa sababu mshikilizi wa afisi hiyo ndiye mshauri mkuu wa serikali katika masuala yote ya kisheria.

Afisa huyo ndiye mshauri wa kisheria wa Rais katika utekelezaji wa majukumu yake kama kiongozi wa taifa na serikali.

Hii ndio maana mshikilizi wa cheo hicho wakati huu, Bw Kihara Kariuki, huketi katika baraza la mawaziri linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta. Kadhalika, Bw Kariuki ni mwanachama wa bodi zote za usimamizi katika mashirika yote ya Serikali.

Lakini inavunja moyo kwamba tangu kuteuliwa kwake mnamo Machi 18, 2018, utendakazi wa Bw Kariuki haujakuwa wa kuridhisha ukilinganishwa na ule wa mtangulizi wake Profesa Githu Muigai, aliyejiuzulu kwa hiari.

Hii ni baada ya serikali kupoteza msusuru wa kesi zilizowasilishwa dhidi yake mahakamani. Isitoshe, baadhi ya maamuzi ya Rais Kenyatta yamekuwa yakibatilishwa na mahakama; hali ambayo inadunisha hadhi ya Afisi ya Rais, kando na kuchangia serikali kupoteza fedha nyingi katika kesi.

Mfano wa hivi punde ni hatua ya wiki jana ya jopo la majaji watano wa Mahakama Kuu kubatilisha mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI). Hatua hii inaudhi ikizingatiwa kuwa mpango huu umegharimu mabilioni ya fedha za mlipa ushuru.

Kimsingi, majaji Profesa Paul Ngugi, George Odunga, Chacha Mwita, Jairus Ngaah na Teresia Matheka, katika uamuzi wa pamoja, walisema Rais Kenyatta alikiuka Katiba na sheria husika kwa kuanzisha mchakato huo. Kinaya ni kwamba kuna Afisi ya Mwanasheria Mkuu nchini yenye wajibu wa kumshauri Rais katika masuala ya kisheria.

Isitoshe, ni mwezi jana tu ambapo Jaji wa Mahakamu Kuu Anthony Mrima aliuamua kuwa Rais alikosea kwa kubuni wadhifa wa Waziri Msaidizi (CAS) na kushikilia kuwa mawaziri sita ambao wanahudumu katika kipindi cha pili cha Jubilee baada ya kuteuliwa tena, walifaa kupigwa msasa na bunge.

Isitoshe, Jaji Mrima aliamua kwamba, ni haramu kwa mtu yeyote kuteuliwa kama Katibu katika wizara yoyote bila kutuma maombi ya kazi hiyo, kuhojiwa kisha jina lake lipendekezwe kwa Rais na Tume ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma (PSC) ndipo ateuliwe katika wadhifa huo.

Mwanasheria Mkuu pia alipoteza kesi ambapo Rais Kenyatta alilaumiwa kwa kukataa kuwaapisha majaji 41 walioidhinishwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Mahakama iliamua mnamo Februari 6, 2021 kuwa, kuchelewesha kwa uteuzi huo kulikuwa kinyume cha sheria na kuamuru majaji hao waapishwe ndani ya siku 14. Ni wazi kuwa Bw Kihara alimpotosha Rais Kenyatta katika suala hili muhimu ambalo sasa limezidisha kero la uhaba wa majaji haswa katika Mahakama ya Rufa.

Kwa misingi, ya mifano niliyotoa hapa, na mingine mingi ambayo nimeacha, naamini kwamba wakati umetimu kwa Rais Kenyatta kumtema Bw Kihara ili kunusuru heshima na hadhi ya serikali na afisi yake.

You can share this post!

TAHARIRI: Sasa serikali ifufue ajenda ya chakula

Idadi ya wateja ingali ya chini katika hoteli kadhaa...