• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:59 AM
CHARLES WASONGA: Murkomen afuatilie jitihada za kudhibiti ajali humu nchini

CHARLES WASONGA: Murkomen afuatilie jitihada za kudhibiti ajali humu nchini

NA CHARLES WASONGA

MIKAKATI iliyotangazwa wiki hii na serikali kwa lengo la kuzuia ajali za barabarani haitazaa matunda ikiwa utepetevu na utovu wa maadili miongoni mwa maafisa wake hautakomeshwa.

Kwa mfano, amri ya Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen kwamba madereva wa magari yote ya uchukuzi wa umma wafanyiwe mtihani mpya wa uendeshaji kuanzia Juni mwaka huu haitasaidia kuzima ajali hizi ikiwa polisi wa trafiki wataendelea kupokea hongo barabarani.

Agizo kwamba magari ya uchukuzi wa umma yakaguliwe upya ili kuondoa yale mabovu halitazaa matunda ikiwa serikali haitahakikisha maafisa wanaoshiriki ufisadi wanakamatwa na kuadhibiwa vikali.

Isitoshe, Bw Murkomen anafaa kushirikiana na mwenzake wa Elimu Ezekiel Machogu kuhakikisha kuwa wasimamizi wa shule wanatekeleza marufuku aliyotangaza dhidi ya safari za mabasi ya shule nyakati za usiku.

Ikumbukwe kuwa amri kama hii imewahi kutolewa na wakuu serikalini katika jitihada za kukomesha ajali zinazohusisha mabasi ya shule. Nakumbuka kuwa mnamo Agosti 7, 2018, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitangaza marufuku hiyo baada ya wanafunzi 11 wa shule ya St Gabriel Academy, iliyoko Mwingi, kufariki basi lao lilipohusika katika ajali ya barabarani eneo la Kanginga, majira ya usiku.

Na Februari 22, mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa usalama, Dkt Fred Matiang’i alisisitiza uwepo wa marufuku hiyo alipoamuru kuadhibiwa kwa mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Tot kufuatia tukio ambapo wanafunzi walishambuliwa na majangili, wakisafiri usiku kwa basi la shule hiyo, karibu na msitu wa Embubut.

Kando na kuwepo kwa sheria kali za trafiki, maarufu kama Sheria za Michuki, utepetevu na ufisadi aghalabu huchangia kutotekelezwa kwazo.

Waziri Murkomen na mwenzake wa Usalama Kithure Kindiki sasa wanapaswa kuhakikisha maafisa wa kikosi cha polisi wa trafiki na wale wa mamlaka ya kitaifa ya usalama barabarani (NTSA), wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa.

Kwa mfano, mamlaka hii inafaa kuhakikisha kuwa magari ya uchukuzi wa umma yanakaguliwa kila mara kuhakikisha kuwa vidhibiti mwendo vinafanya kazi sawasawa sawa na mikanda ya usalama.

NTSA inafaa kuwakuchukulia hatua kali madereva wa magari hayo ambayo huvuruga vifaa hivyo ili wapitishe kasi inahitajika ya kilomita 80 kwa saa.

Kando na hayo, itabidi Waziri Murkomen aige mfano wa aliyekuwa waziri wa Uchukuzi marehemu John Michuki ambaye mwenyewe alikuwa akijitokeza barabarani kukagua utekelezaji wa sheria za trafiki.

Inakera kwamba ndani ya kipindi cha wiki mmoja pekee zaidi ya watu 22 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani ambazo zinaweza kuepukika huku zaidi ya watu 2,000 wakiangamia kwa njia hiyo tangu Januari mwaka huu

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mafunzo hatari ya kiroho ni tishio kwa jamii,...

WANTO WARUI: Waziri wa Elimu aweke mikakati kabambe kulinda...

T L