• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kufuturu kwa tende kuna manufaa mengi kiafya

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kufuturu kwa tende kuna manufaa mengi kiafya

NA ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii tukufu na bora tukiwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ili kukumbushana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu. Ubora na utukufu huo ukizidi mno hasa katika kipindi hiki cha saum, kwenye ibada hii muhimu mno, miongoni mwa nguzo mojawapo wa nguzo tano kuu za dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote tuchukue uzito wa nafasi hii kumshukuru sana Mola wetu, Allah (SWT) ambaye ametujaalia kukutana, kuwa hai, kufanya ibada na kufaidi fadhila za ibada hii ya saumu.

Vivyo hivyo, twachukua nafsi na satua hii adhimu kumtilia dua na kumfanyia maombi kipenzi chetu, kigezo chetu na mfano wetu bora, mwalimu na mwombezi wetu Mtume (SAW).

Mengi yamesemwa na yanazidi kusemwa kutoka kwa walimu, mashekhe na maustadh wetu kuihusu funga ya mwezi huu wa Ramadhan. Leo hii, ningependa tuangazie umuhimu wa kulishana. Kufuturishana kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

Wengi wetu, ndugu, jamaa na marafiki tumekuwa tukialikana. Inafaa tuzidi kualikana zaidi ili sio tu kuunganisha jamii, kusahau tofauti zetu zilizopo za makabila, siasa, rangi, dini, huku tukifaidi kutokana na kuufunga huku.

Kama anavyosema Shekhe Hassan Omar Kinyua ni kuwa ukimlisha mwenziyo aliyefunga, ni kuwa nyote mnafaidi. Mwenye kulishana na huyo mwenye kulishwa.

Hizi hapa baadhi ya aya za vifungu kwenye Kurani kuhusiana na kula huku: “Enyi watu kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shetani, bila shaka yeye kwenu ni adui dhahiri (Quran: 2:168). “Enyi Mlioamini kuleni vizuri tulivyokuruzukuni, na Mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa mnamuabudu yeye peke yake”. (Quran: 2:172). “Na kuleni katika vile alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu vilivyo vizuri na halali na Mcheni Mwenyezi Mungu ambaye nyinyi mnamwamini (Quran: 5: 88). “…… na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri). Lakini msipite kiasi tu. Hakika yeye (Mwenyezi Mungu) hawapendi wapitao kiasi.” (Quran; 7:31).

Ingawa hivyo, tuchukue nafasi hii kutahadharishana dhidi ya baadhi yetu ambao hufanya israfu wakati wa kula au kufuturishana. Haimaanishi kuwa Ramdhan ni mwezi wa kula na kunywa tu. La hasha! Huu ni mwezi wa ibada.

Mtume Muhammad (SAW) amehimiza sana watu wawe wanapima vyakula vyao. Pia, Mtume (S.A.W) amefundisha kuwa mtu akila aligawe tumbo lake sehemu tatu. Sehemu ya kwanza iwe nafasi ya chakula, ya pili maji, na ya tatu nafasi ya kuweza kupumua (hewa). Vile vile, Mtume (s.a.w) amesema mtu akila aache hali ya kuwa kidogo anasikia njaa. Kwa hakika kama tungekuwa tunafanya uchaguzi sahihi wa vyakula vyetu, kuwa na tania nzuri ya ulaji na kula kwa kiasi kama Mwenyezi Mungu na Mtume wake walivyotufundisha tunge weza kufikia lengo la pili la funga ambalo ni kuimarisha afya ya kiwiliwili.

Kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W), mfungaji anatakiwa afungue kwa tende au maji, halafu aswali magharibi na baada ya hapo aendelee kula. Na hapa ndipo tunaposema kukata swaum na kula futari.

Mtume (S.A.W) na Maswahaba zake walivyokuwa wanakula tende za kufuturu ni witiri (1, 3, 5, 7, n.k).

Zaidi ya hayo, tukumbuke msisitizo wa Mtume (s.a.w) wa kuwahi kufuturu mara tu muda unapofika. “Watu wataendelea kuwa katika heri endapo tu watakuwa wanaharakisha kufuturu (Sahih Bukhari na Sahih Muslim) ”.

Kufuturu kwa tende ni jambo lenye faida kubwa kama alivyohimiza Mtume (s.a.w). Maendeleo ya sayansi yanatusaidia kuongeza ufahamu wetu unaosema kuwa tende ni chakula na pia ni tunda lenye dhamani kubwa sana kwa binadamu.

Mtu akila tende aina hii ya sukari inanyonywa na utumbo na kuunguzwa na seli na hatimae inatoa nguvu kwa haraka. Kwa mfungaji swaum nguvu hii humpa furaha na akili yake inatuama kwa haraka. Tende pia ina vitamini aina ya C kiasi cha gramu 3, na kiasi kidogo cha vitamini B-complex. Tende zikiwa hazijawiva sana na mbichi (fresh) ndio zina vitamini nyingi zaidi. Aina hii ndiyo aliyokuwa anaitumia sana Mtume wetu (S.A.W).

Ijumaa Kareem!

Saum maqbul

[email protected]

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Walimu wanawasaliti wazazi kupendekeza karo...

MAKALA MAALUM: Aliyesingiziwa akafungwa maisha asherehekea...

T L