• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
TAHARIRI: Heko za dhati wanamichezo kwa kuchochea chipukizi nchini

TAHARIRI: Heko za dhati wanamichezo kwa kuchochea chipukizi nchini

NA MHARIRI

TIMU ya taifa ya ndondi ‘Hit Squad’ ilivuma katika mashindano ya Afrika Zoni ya tatu nchini DRC kwa kushinda jumla ya medali 18 na kumaliza katika nafasi ya pili.

Mabondia wa Kenya walishamiri sana katika mapigano yao wakishinda medali sita za dhahabu, tano za fedha na saba za shaba.

Ni matokeo yanayostahili pongezi baada ya mabondia hao kuizolea taifa sifa kedekede baada ya kusuasua kwa kipindi kirefu katika mashindano ya kimataifa.

Kinyume na matokeo ya mashindano ya mwaka jana ambapo Kenya ilipata jumla ya medali 12 ikiwemo moja pekee ya dhahabu,tano za fedha na sita za shaba.

Kulingana na mkufunzi Duncun ‘Sugar Ray’ Kuria, maandalizi mazuri, ushirikiano mzuri baina ya Shirikisho la Ndondi Nchini (BFK), Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (Nock) na Wizara ya michezo ulichangia pakubwa matokeo mazuri katika mashindano hayo.

Shirika la ndondi nchini BFK ilihakikisha mabondia wa timu ya taifa wanashiriki mashindano ya kujipima nguvu kabla ya kuanza rasmi maandalizi yao wiki tano kabla ya mashindano ya DRC.

Ni wakati muafaka kwa mashirikisho mengine ya michezo nchini kuiga mfano mzuri wa BFK kwa kuwaweka wanamichezo wao katika mazingira mazuri wanapojiandaa kupeperusha bendera ya taifa kimataifa.

Mbali na nchi yetu kutambulikana katika viwango vya kimataifa na pia kuinua utalii, lililo bora zaidi ni jinsi fanaka za wanamichezo hawa zinavyowachochea vijana wetu ili kuwaiga na hatimaye kuwa wachezaji wa kimataifa siku za usoni.

Si ajabu siku hizi michezo imegeuka kuwa mojawapo wa mbinu za chipukizi kujipatia riziki kupitia mapato yanayotokana nayo.

Kando na mabondia wetu, wanariadha wetu walishamiri katika mbio za Boston Marathon, Massachusetts, Amerika ambapo Peres Jepchirchir alishinda kitengo cha wanawake mapema wiki hii.

Naye Evans Chebet alishinda mbio hizo hizo upande wa wanaume.

Mwezi wa Februari dereva barobaro Mcrae Kimathi alishiriki mbio za magari kwenye barafu nchini Uswidi na kufanya vyema hata ingawa hakuwa mshindi wa mbio hizo.

Mwezi uliopta, dereva wa kike Maxine Wahome alishinda mbio za magari kitengo cha wanawake. Huku tukimiminia sifa tele wazalendo na mashujaa hawa wetu katika michezo, ni matumaini yetu kwamba bidii zao zitaongezeka ili kuzidi kupaishi ari ya vijana wetu na kuwapa matumaini siku za usoni hasa kiuchumi, kimaadili na kisaikolojia.

You can share this post!

Kibaki kuzikwa Jumamosi, Aprili 30, 2022

KCSE 2021: Jeriel Ndeda Obura kutoka Mang’u High...

T L