• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
TAHARIRI: Wasiolipa Helb wafuatiliwe na kuhimizwa kulipa ili wafae wengine

TAHARIRI: Wasiolipa Helb wafuatiliwe na kuhimizwa kulipa ili wafae wengine

NA MHARIRI

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) kwa miaka mingi imewawezesha wanafunzi wengi kulipia masomo yao ya chuo kikuu.

Imekuwa muhimu hasa kwa wanafunzi walio wengi kutoka familia maskini, ambao wasingeweza kuafiki ndoto yao ya mafunzo ya ngazi ya juu katika taasisi za elimu ya juu.

Wanaonufaika na mkopo huo huhitaji kupasi vyema mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne kisha kujitwalia nafasi chuoni, halafu wanaweka ombi la kupewa mkopo kutoka kwa Helb.

Hapo awali, mikopo hiyo ilipatikana kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma pekee.

Kadiri Helb ilivyozidi kukomaa na kuwa na ufanisi zaidi, mpango huo ulipanuliwa hadi kwa vyuo vikuu vya kibinafsi na vyuo vya elimu ya juu. Hali ilikuwa shwari hadi miaka kadhaa iliyopita, wakati Helb ilipoanza kupata matatizo.

Kwanza, ufadhili kutoka Hazina ya Kitaifa umepungua huku mahitaji ya mikopo yakiongezeka nafasi nyingi za vyuo vikuu zikizidi kupatikana nchini.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wamekuwa wakiwania mikopo inayopungua. Ufadhili wa elimu ya juu umeathiriwa sana na hali mbaya ya kiuchumi iliyochochewa na athari mbaya za janga la Covid-19.

Miaka miwili iliyopita wakati nchi ilikuwa imefungwa pamoja na na vizuizi vingine vimevuruga uchumi, na kusababisha Hazina ya Kitaifa kutokuwa na uwezo wa kuongeza ufadhili kwa mashirika ya umma.

Na wanaobeba mzigo mkubwa ni wanafunzi ambao hawawezi kulipia masomo na utunzaji wao.

Kwa nakisi ya bajeti ya Sh3.2 bilioni, Helb imekuwa ikikopesha wanafunzi kiasi kidogo mno.

Idadi kubwa ya watumaji maombi 75,000 hawakupata chochote huku wachache waliobahatika wakitunukiwa kiasi cha kutosha.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Helb, Charles Ringera, mwaka huu wa fedha, Helb ilitarajia wanafunzi 236,555 wa vyuo vikuu kutuma maombi ya mikopo ya Sh10.2 bilioni lakini iliishia na waombaji 269,000.

Pia ilitarajia wanafunzi 162,147 wanaoendelea kuomba mikopo na ilikuwa tayari kutoa Sh7 bilioni lakini idadi hiyo ilizidiwa na takriban maombi 15,000.

La kushangaza ni kwamba, baadhi ya wanufaika wa zamani wanadaiwa Helb mabilioni ya shilingi.

Ni lazima wafuatiliwe ili washinikizwe kulipa madeni yao.

Pili, kuna haja ya ubunifu ili kuongeza ufadhili wa elimu kutoka kwa wahisani binafsi na mashirika ya kibinafsi.

You can share this post!

Liverpool yaponda Man-United na kutua kileleni mwa jedwali...

Mahakama yakataa kuharamisha sheria ya vyama vya kisiasa

T L