• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 9:50 AM
Arsenal wacharaza Newcastle United 2-0 katika EPL

Arsenal wacharaza Newcastle United 2-0 katika EPL

Na MASHIRIKA

PIERRE-EMERICK Aubameyang alifunga bao katika mchuano wake wa kwanza tangu apone kutokana na malaria na kuongoza Arsenal kuwapepeta Newcastle United 2-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili uwanjani St James’ Park.

Kiungo Mohamed Elneny alifunga bao lake la kwanza la EPL akivalia jezi za Arsenal katika dakika ya tano kabla ya Aubameyang kuwazamisha wenyeji wao kunako dakika ya 66. Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Aubameyang ambaye ni raia wa Gabon kusakatia Arsenal tangu Aprili 3, 2021.

Akihojiwa na wanahabari mwishoni mwa mechi, Aubameyang alikuwa mwingi wa sifa kwa madaktari waliomshughulikia hospitalini.

Ni matarajio ya kocha Mikel Arteta kwamba ushindi dhidi ya Newcastle sasa utawapa masogora wake motisha zaidi ya kupepeta Villarreal ya kocha Unai Emery katika marudiano ya nusu-fainali ya Europa League mnamo Alhamisi ya Mei 6, 2021 ugani Emirates. Arsenal watashuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakilenga kubatilisha kichapo cha 2-1 walichopokezwa na Villarreal katika mkondo wa kwanza nchini Uhispania mnamo Aprili 29, 2021.

Chini ya kocha Steve Bruce, Newcastle walikamilisha mchuano wao dhidi ya Arsenal wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Fabian Schar kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea visivyo fowadi Gabriel Martinelli aliyechangia bao la pili la Arsenal.

Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 49, moja pekee mbele ya Aston Villa ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na Arsenal.

Kwa upande wao, Newcastle wanakamata sasa nafasi ya 17 kwa pointi 36 sawa na Burnley. Ni pengo la alama tisa pekee ndilo linawatenganisha Newcastle na Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi baada ya Sheffield United.

Newcastle watavaana na Leicester City katika mchuano wao ujao mnamo Ijumaa ya Mei 7, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Messi afunga mabao mawili na kuongoza Barcelona kucharaza...

Ronaldo awabeba Juventus dhidi ya Udinese katika Serie A