• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Arsenal watoka nyuma kwa mabao matatu na kuwalazimishia West Ham sare ya 3-3 katika EPL

Arsenal watoka nyuma kwa mabao matatu na kuwalazimishia West Ham sare ya 3-3 katika EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL walitoka nyuma kwa mabao matatu kwa nunge na kujizolea alama moja muhimu baada ya kuwalazimishia West Ham United sare ya 3-3 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili usiku.

Chini ya kocha David Moyes, West Ham walifunga mabao matatu ya haraka chini ya dakika 32 za kipindi cha kwanza kupitia kwa Jesse Lingard, Jarrod Bowen na Tomas Soucek aliyejaza kimiani krosi ya Michail Antonio.

Arsenal walijipa matumaini ya kurejea mchezoni kupitia kwa Soucek aliyejifunga mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kuzidiwa ujanja na mpira ulioelekezwa langoni mwao na fowadi Alexandre Lacazette.

Beki Craig Dawson wa West Ham alijifunga pia katika dakika ya 61 baada ya kushindwa kudhibiti krosi ya difenda wa Arsenal, Calum Chambers.

Arsenal walifunga karamu yao ya mabao katika kipindi cha pili kupitia kwa Lacazette aliyejaza wavuni krosi ya fowadi Nicolas Pepe katika dakika ya 82.

Matokeo ya mechi hiyo yalisaza West Ham katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 49, mbili pekee nyuma ya nambari nne Chelsea.

Arsenal kwa upande wao, wanajivunia alama 42 na walipoteza nafasi nzuri ya kuwakaribia Everton, Tottenham Hotspur na Liverpool ambao pia wanawania nafasi ya kunogesha soka ya bara Ulaya muhula ujao.

Ushindi kwa West Ham ungaliwashuhudia wakifikia Chelsea kwa idadi ya alama ila wangesalia bado katika nafasi ya tano kutokana na uchache wa mabao yao.

Japo West Ham hawajawahi kukamilisha kampeni za EPL mbele ya Arsenal tangu 1985-86, pengo la alama saba bado linatamalaki kati yao huku zikisalia mechi tisa pekee kwa kampeni za msimu huu wa 2020-21 kukamilika rasmi.

Ingawa Arsenal wangali na matumaini finyu ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora, dalili zote zinaashiria kwamba watalazimika kutumia kipute cha Europa League kama njia rahisi na yenye uhalisia zaidi kufuzu kwa gozi la UEFA muhula ujao.

Japo wanashuhudia ufufuo mkubwa wa makali yao chini ya Moyes, rekodi ya West Ham dhidi ya Arsenal bado ni duni. Kikosi hicho kimeshinda mechi nane pekee kati ya 42 zilizopita dhidi ya Arsenal ambao wamewazamisha mara 32 na kuambulia sare mara 10.

Arsenal waliingia ugani kupepetana na West Ham wakijivunia motisha ya kubandua Olympiakos ya Ugiriki kwenye hatua ya 16-bora ya Europa League na kufuzu kwa robo-fainali ya mikondo miwili itakayowakutanisha Slavia Prague.

Iwapo watawabwaga miamba hao wa soka kutoka Jamhuri ya Czech, basi Arsenal watapepetana ama na Dinamo Zagreb ya Croatia au Villarreal ya Uhispania kwenye hatua ya nusu-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Droo ya masumbwi ya Kinshasa yafanywa mataifa manne...

Chelsea wapewa Man-City huku Leicester wakionana na...