• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 6:55 AM
Benzema awabeba Real Madrid dhidi ya Celta huku Sevilla na Valladolid wakiambulia sare La Liga

Benzema awabeba Real Madrid dhidi ya Celta huku Sevilla na Valladolid wakiambulia sare La Liga

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Karim Benzema alizititiga nyavu katika mechi ya sita mfululizo, mabao yake mawili yakiwezesha Real Madrid kucharaza Celta Vigo 3-1 katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Benzema ambaye sasa amefungia Real jumla ya mabao 23 msimu huu, alichangia goli la tatu la waajiri wake lililotiwa wavuni na kiungo Marco Asensio.

Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real wanajivunia alama 60, tatu zaidi kuliko nambari nne Sevilla iliyolazimishiwa na Real Valladolid sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya La Liga. Zimesalia mechi 10 pekee kwa kampeni za La Liga muhula huu kukamilika rasmi.

Real ambao hawajapoteza mechi yoyote kati ya 10 zilizopita ugenini, walijibwaga ugani kumenyana na Celta Vigo wakijivunia motisha ya kubandua Atalanta ya Italia kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa jumla ya magoli 4-1 na kufuzu kwa robo-fainali itakayowakutanisha na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool.

Wakicheza dhidi ya Valladolid, kipa Yassine Bounou, 29, alisawazishia Sevilla mwishoni mwa kipindi cha pili na akaonyeshwa kadi ya manjano baada ya kuvua jezi alipokuwa akisherehekea goli lake.

Bounou ambaye ni raia wa Canada, ndiye kipa wa kwanza kuwahi kufungia Sevilla bao tangu Andres Palop afanye hivyo kupitia kichwa katika mechi ya Europa League iliyowakutanisha na Shakhtar Donetsk mnamo 2006-07.

Bounou ndiye kipa wa pili katika La Liga kufunga bao msimu huu baada ya Marko Dmitrovic wa Eibar kufanya hivyo kupitia penalti dhidi ya Atletico Madrid mnamo Januari 2021. Mara ya mwisho kwa makipa wa vikosi vya La Liga kufunga mabao ligini ilikuwa mwaka wa 1987.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Benevento yadidimiza matumaini ya Juventus kutwaa taji la...

Spurs wapepeta Aston Villa na kupaa hadi nafasi ya sita...