• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Boit, Kandie kujaribu kubwaga Cheptegei na Mo Farah Olimpiki

Boit, Kandie kujaribu kubwaga Cheptegei na Mo Farah Olimpiki

Na CHRIS ADUNGO

SIKU chache baada ya kuambulia pakavu kwenye mbio za kilomita 10 za Great Ethiopian Run jijini Addis Ababa, mwanariadha Solomon Boit sasa amefichua azma ya kuhamia mbio za mita 10,000 kwa watu wazima.

Boit aliyetupwa hadi nafasi ya 21 kwenye kivumbi cha Ethiopia kilichotamalakiwa na wenyeji, amesema maazimio yake sasa ni kutwaa dhahabu ya mita 10,000 kwenye Olimpiki za Tokyo, Japan mwaka huu.

Kennedy Kimutai (29:50.16) na Evans Kipkemei (30:50.66) waliokuwa wawakilishi wengine wa Kenya nchini Ethiopia waliambulia nafasi za 27 na 35 mtawalia.

“Nilikubaliana na kocha wangu kwamba mbio za Great Ethiopia Run ndizo zangu za mwisho barabarani. Sasa napania kurejea uwanjani kunogesha Olimpiki,” akasema mtimkaji huyo ambaye hushiriki mazoezi yake katika eneo la Iten chini ya uelekezi wa kocha veterani, Colm O’Connell.

Boit aliwahi kushiriki mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2018 na kuambulia nafasi ya nne jijini Tampere, Finland.  Rhonex Kipruto ambaye pia ameanika azma ya kutua Japan, alitwaa dhahabu kwenye mbio hizo za Finland.

Mkenya mwingine ambaye ameapa kupigania nafasi ya kupeperusha bendera ya Kenya nchini Japan ni Kibiwott anayeshikilia rekodi ya dunia ya Half Marathon.

Kikosi cha Kenya kinatarajiwa kuunda njama ya kumpiku Joshua Cheptegei wa Uganda ambaye ametangaza kwamba atakuwa akiwania nishani mbili za dhahabu katika mbio za kilomita 5,000 na kilomita 10,000 kwenye Olimpiki.

Cheptegei, 24, alivunja rekodi za dunia kwenye fani hizo mbili mnamo 2020. Alisajili muda wa dakika 26:11 kwenye mbio za 10,000 mnamo Oktoba jijini Valencia na kuivunja rekodi ya dakika 26:17.53 iliyowekwa na Mwethiopia Kenenisa Bekele mnamo 2005.

Miezi miwili kabla ya ufanisi huo, Cheptegei alikuwa amevunja pia rekodi ya miaka 16 ya dakika 12:37 iliyowekwa na Bekele kwenye mbio za mita 5,000 kwa kusajili muda wa dakika 12:35.36 kwenye Monaco Diamond League jijini Paris, Ufaransa.

Iwapo Cheptegei ambaye huvalia viatu aina ya Dragonfly kutoka kampuni ya Nike atatwaa medali za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 jijini Tokyo mwakani, basi atakuwa mwanariadha wa nane kwa upande wa wanaume kuwahi kufikia rekodi hiyo kwenye fani hizo mbili.

Kandie amesema anajifua vilivyo kwa nia ya kutwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki japo hajawahi kushiriki mbio hizo ambazo zimekuwa zikitamalakiwa na Bekele pamoja na Mwingereza Mo Farah katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Farah ambaye ni bingwa mara nne wa Olimpiki, amethibitisha kwamba hatakuwa sehemu ya wanariadha watakaonogesha mbio za mita 5,000 jijini Tokyo ila atalenga kuhifadhi ufalme wake kwenye mbio za mita 10,000 – hatua itakayofanya fani hiyo kuwa ya kusisimua zaidi.

“Sijawahi kushiriki mashindano ya mita 10,000 lakini nahisi kwamba nina uwezo wa kubwaga Mo Farah na Cheptegei katika fani hiyo ndiposa nitawania fursa ya kuwa sehemu ya kikosi kitachopeperusha bendera ya Kenya jijini Tokyo,” akasema.

Kwa mujibu wa kalenda mpya ya msimu wa 2021 iliyotolewa na mkurugenzi wa michezo katika Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Paul Mutwii, uteuzi wa kikosi kitakachowakilisha Kenya nchini Japan katika mbio za mita 10,000 utafanywa Juni 26-27, 2021 jijini Nairobi.

“Kushiriki mbio hizi kutachangia kuimarika kwa kasi yangu kadri ninavyolenga kuvunja rekodi yangu ya nusu marathon kwa kusajili muda wa chini ya dakika 56:00 kwenye mbio za kilomita 21 mwaka huu. Hili ni jambo ambalo nimekuwa nikilijaribu mazoezini na ninaamini linawezekana,” akaongeza Kandie aliyetumia Valencia Half Marathon kuvunja rekodi ya awali ya dunia ya nusu marathon (58:01) iliyowekwa na Mkenya Geoffrey Kamworor jijini Copenhagen, Denmark mnamo 2019.

“Tangu mwaka wa 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala mbio hizo mita 10,000 katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika fani hiyo. Tunalenga kutafuta suluhu katika mbio za mita 10,000 na mita 5,000 ambazo Kenya haijashinda kwa upande wa wanaume kwa muda mrefu,” akasema Mutwii.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini mnamo 1988

  • Tags

You can share this post!

Kura za Bobi Wine zaongezeka

Bruno Fernandes aweka rekodi EPL