• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
CAVB yathibitisha Kenya imeingia Kombe la Voliboli Afrika

CAVB yathibitisha Kenya imeingia Kombe la Voliboli Afrika

Na GEOFFREY ANENE

Shirikisho la Voliboli Afrika (CAVB) limetangaza orodha ya washiriki wa Kombe la Afrika la wanaume pia wanawake la voliboli.

Kenya ni miongoni mwa mataifa 20 ya wanaume na 16 ya wanawake ambayo yametoa ithibati ya kuwania mataji hayo nchini Rwanda mwezi ujao mnamo Septemba 5-20.

Mabingwa mara tisa Malkia Strikers, ambao wamerejea majuzi kutoka Olimpiki 2020, watafahamu wapinzani wao wa mechi za makundi kutoka kwa orodha ya Burundi, Ivory Coast, DR Congo, Ethiopia, Gambia, Guinea, Morocco, Nigeria, Rwanda, Senegal, Tanzania, Tunisia, Zambia na mabingwa watetezi Cameroon pamoja na mahasimu wa tangu jadi Misri.

Timu za wanaume zinajumuisha Burundi, Burkina Faso, Ivory Coast, Cameroon, DR Congo, Misri, Ethiopia, Gambia, Guinea, Kenya, Mali, Morocco, Niger, Nigeria, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na mabingwa watetezi Tunisia.

Majuzi, Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) lilitangaza kuwa lina mipango ya kuingiza timu zake zote mbili katika mashindano hayo.

Kocha wa Malkia Strikers, Paul Bitok alinukuliwa akisema kuwa ataongeza wachezaji wawili katika kikosi chake cha wachezaji 12 kilichozabwa na Japan, Korea Kusini, Serbia, Dominican na Brazil kwa seti 3-0 mfululizo katika mechi za Kundi A ikimaliza nafasi ya 12 (mkiani).

Vipusa wa Bitok walizoa medali ya fedha katika makala mawili yaliyopita ya Kombe la Afrika baada ya kuchapwa na Cameroon katika fainali. Wanaume wa Kenya hawajawahi kushiriki mashindano makubwa kuliko yale ya Afrika. Hawakushiriki makala yaliyopita ya dimba la Afrika mwaka 2019. Pia, hawajawahi kupata medali.

  • Tags

You can share this post!

Shahbal ‘avuka kisiki’ katika urithi wa Joho

PSG yajiandaa kumchukua Messi