• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
Chepkirui, Cherotich wang’ara mbio za mita 5,000 riadha za AK zikiingia duru ya pili Kasarani

Chepkirui, Cherotich wang’ara mbio za mita 5,000 riadha za AK zikiingia duru ya pili Kasarani

Na AYUMBA AYODI

Bingwa wa Afrika mbio za mita 5,000 mwaka 2016 Sheila Chepkirui na Daisy Cherotich walitawala vitengo vyao vya mbio za mita 5,000 katika duru ya pili ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) uwanjani Kasarani, Ijumaa.

Hata hivyo, Cherotich kutoka mjini Kapsabet ndiye alibahatika kutwaa taji la pili mfululizo akiandikisha kasi ya juu kabisa ya dakika 15 na sekunde 26.7 na kumbwaga Beth Chepkemoi pia kutoka Kapsabet (15:37.7).

Naomi Chepng’eno kutoka Nakuru alikamilisha katika nafasi ya tatu kwa 15:42.5

“Nililenga kutimka chini ya dakika 15, lakini upepo haukuniruhusu,” alisema Cherotich, ambaye alinyakua taji la mbio za mita 10,000 katika duru ya kwanza ugani Nyayo mnamo Februari 28.

“Mbio za mita 5,000 si zangu. Nazishiriki tu kutafuta kasi ya mbio za mita 10,000 ambazo natumai kupata tiketi ya kuwakilisha Kenya kwenye Olimpiki jijini Tokyo,” alisema Cherotich.

Akitimka mbio zake za kwanza tangu akamilishe mbio za nyika za majeshi (KDF) katika nafasi ya tatu mwezi Januari, Chepkirui alimlemea kwa kasi bingwa wa dunia wa mbio za nyika za kitengo cha chipukizi Beatrice Chebet katika hatua za mwisho akiibuka mshindi kwa dakika 15:29.8.

Chebet aliridhika katika nafasi ya pili (15:30.6) naye Mary Munanu akakamilisha katika nafasi ya tatu (15:52.2).

“Sikuwa nataka muda huu, lakini nahisi vizuri kuibuka mshindi. Bado nahitaji kuimarisha kasi yangu ninapolenga kushiriki Olimpiki,” alisema Chepkirui anayetumai kupeperusha bendera ya Kenya kwenye Olimpiki katika mbio za mita 5,000.

Peter Mwaniki kutoka Nanyuki, Alexander Mutiso (Makueni) na Emmanuel Kemboi walishinda vitengo vyao vya mbio za mita 10,000.

Mwaniki alishinda kitengo chake kwa kasi ya juu ya dakika 28:42.88 akifuatiwa na Alfred Barkach kutoka KDF (28:43.1).

Mutiso alitamba katika kitengo cha tatu kwa dakika 28:50.15 huku Edmond Kipng’etich kutoka Kericho akimfuata kwa 29:03.02.

Kemboi alishinda kitengo cha pili kwa dakika 29:12.99, lakini muda huo wake ulikuwa wa tisa-bora. Alikamilisha mbele ya Gilbert Kimunyan kutoka Torongo (29:14.29).

Dominic Tabunda kutoka KDF alishinda fani ya ‘hammer’ kwa mtupo wa umbali wa mita 57.27 naye Lucy Omondi akawa mshindi kwa upande wa kinadada kwa mtupo wa mita 49.10.

Tera Langat kutoka Idara ya Magereza aling’ara katika fani ya kuruka umbali baada ya kuandika mita 7.46.

Maximilla Imali kutoka Idara ya Polisi aliandikisha kasi ya juu kabisa katika mbio za mita 100 za kinadada alipokamilisha umbali huo kwa sekunde 11.80 naye Ferdinand Omanyala akawa na kasi ya juu kabisa katika kitengo cha wanaume (sekunde 10.41).

TAFSRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Sina uhakika iwapo Sergio Ramos atasalia kambini mwa Real...

Waqo akaidi tena mwaliko wa PIC