• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:42 PM
Sina uhakika iwapo Sergio Ramos atasalia kambini mwa Real Madrid – Zidane

Sina uhakika iwapo Sergio Ramos atasalia kambini mwa Real Madrid – Zidane

Na MASHIRIKA

KOCHA Zinedine Zidane wa Real Madrid amesema hana uhakika iwapo beki na nahodha Sergio Ramos ataendelea kuwa mchezaji wa kikosi hicho msimu ujao.

Mkataba wa sasa kati ya Real na Ramos, 34, unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21. Ramos alisajiliwa na Real kutoka Sevilla ambao pia ni washiriki wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo 2005.

Nyota huyo raia wa Uhispania anajivunia kuwaongoza Real kutia kapuni mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), manne ya Kombe la Dunia na matano ya La Liga katika kipindi cha miaka 16 ambayo amehudumu uwanjani Santiago Bernabeu.

“Nataka kuwa mkweli, na lazima nisema kwamba sijui chochote kuhusu mustakabali wake kwa sasa na kitakachomfanyikia,” akatanguliza Zidane ambaye ni raia wa Ufaransa.

“Tungependa sana asalie hapa ili aendelee kuwa mchezaji wetu. Ni miongoni mwa wachezaji muhimu zaidi kikosini na ndiyo maana ningependa sana awe sehemu ya kampeni za Real katika misimu kadhaa ijayo. Hivyo ndivyo ningesema kama kocha,” akaelezea Zidane ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Real.

Kufikia sasa, Ramos anajivunia rekodi ya kufungia Real jumla ya mabao 100 kutokana na mechi 668 za mashindano mbalimbali.

Wakati uo huo, Zidane amedokeza kuhusu uwezekano wa nyota Cristiano Ronaldo kurejea kambini mwa Real mwishoni mwa msimu huu iwapo waajiri wake wa sasa Juventus watashindwa kuhifadhi ufalme wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Italia, Juventus watakuwa radhi kumwachilia Ronaldo mwishoni mwa muhula huu baada ya nyota huyo raia wa Ureno kushindwa kuwatambisha kwenye gozi la UEFA kwa mara nyingine msimu huu. Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus walibanduliwa na FC Porto ya Ureno kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.

Kwa upande wao, Real kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 54, nane nyuma ya viongozi Atletico Madrid. NI pengo la alama mbili ndilo linatenganisha Real na nambari mbili Barcelona.

“Kila mtu anafahamu Ronaldo ni nani katika historia ya kikosi cha Real. Aliongoza kikosi kujivunia mafanikio mengi akivalia jezi zao. Kila kitu alichokifanya kambini mwa kikosi hicho kilikuwa shwari na kiliwagusa sana mashabiki. Siwezi kusema zaidi ya hapo kwa sasa kwa kuwa angali mchezaji wa Juventus ambao tunawaheshimu sana,” akafafanua Zidane.

Mbali na Real, Ronaldo anahusishwa pia na uwezekano wa kutua kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) ambao ni miamba wa soka nchini Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii wakerwa na agizo la...

Chepkirui, Cherotich wang’ara mbio za mita 5,000...