• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
CORONA: Liverpool hawawezi kusafiri Ujerumani kwa mchuano wa UEFA

CORONA: Liverpool hawawezi kusafiri Ujerumani kwa mchuano wa UEFA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL hawataweza kusafiri hadi Ujerumani kwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya RB Leipzig mnamo Februari 2021.

Ujerumani imepiga marufuku wageni kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Uingereza, kutokana na kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi vya corona.

Taarifa kutoka Wizara ya Usalama nchini Uijerumani ilishikilia kwamba Leipzig wanaoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wameelezwa kwamba mchuano huo haujafikia viwango vya kuruhusu kulegezwa kwa kanuni zilizopo kwa sasa za kukabiliana na maambukizi ya janga la corona.

Kwa upande wao, Uefa wamesema kwamba wangali katika mawasiliano ya mara kwa mara na vikosi husika vinavyotarajiwa kunogesha kivumbi hicho.

Liverpool nao watakuwa wakiarifiwa mara kwa mara kuhusu mabadiliko yoyote kuhusiana na mchuano huo.

Vinara wa Uefa wametoa kanuni mpya kuhusu jinsi mechi za hatua ya mwondoano za UEFA na Europa League zitakavyopigwa wakati huu wa janga la corona.

Iwapo kanuni zinazolenga kudhibiti maambukizi katika taifa fulani zitazuia mechi kupigwa, klabu iliyokuwa mwenyeji wa mchuano huo italazimika kupendekeza sehemu nyingine mbadala (nchi tofauti) ya kupigiwa kwa mechi husika.

Hata hivyo, iwapo klabu iliyokuwa ichezee nyumbani itashindwa kufanya hivyo na pasiwe na uwezekano wowote mwingine wa kupigwa kwa mechi husika, basi kikosi cha nyumbani kitachukuliwa kuwa kimeshindwa kwa mabao 3-0.

Kwa kuwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa UEFA kati ya Leipzig na Liverpool umepangiwa kupigwa Februari 17, upo uwezekano wa mpangilio wa mechi hiyo kubadilishwa hivi kwamba Liverpool wawe wenyeji wa mkondo wa kwanza kisha Leipzig wawe waandalizi wa mechi ya marudiano mnamo Machi 10, 2021 wakati ambapo baadhi ya kanuni za kudhibiti msambao wa corona nchini Ujerumani zitakuwa zimelegezwa.

Hata hivyo, Uefa huenda ikaamua kivumbi hicho kipigwe kwa kanuni za mikondo miwili (nyumbani na ugenini) katika nchi tofauti au kipute chenyewe kiwe cha mkondo mmoja pekee katika nchi nyingine tofauti.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chelsea wabomoa Spurs

Museveni akabidhiwa nakala za kesi ya Bobi Wine kutaka...