• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Covid-19 yawapunguzia utamu mashabiki wa mbio za magari Kenya

Covid-19 yawapunguzia utamu mashabiki wa mbio za magari Kenya

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Mbio za Magari Kenya (KMSF) limepiga marufuku mashabiki Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) za duru ya KCB Machakos Rally hapo Machi 28 pamoja na mashindano mengine yote inayosimamia.

Tangazo hilo limetolewa miezi mitatu kabla ya Kenya kuandaa duru ya Mbio za Magari ya Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 19.

Mbio za Safari Rally, ambazo zilikuwa kwenye ratiba ya Mbio za Magari za Dunia (WRC) mara ya mwisho mwaka 2002, zimeratibiwa kurejea katika ulingo wa dunia mnamo Juni 24-27 zikifanyika katika kaunti za Nairobi na Nakuru.

Wapenzi wa Safari Rally, ambayo inatarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki na kusimamiwa na maafisa zaidi ya 2,200, huenda wakaonea mashindano hayo kwenye runinga tu hali ya janga la virusi vya corona isipoimarika.

Kenya kwa wakati huu inashuhudia wimbi la tatu la janga hilo. Kupitia Mkurugenzi wa KMSF Jim Kahumbura, shirikisho hilo limetangaza Machi 24 kuwa halitaruhusu kabisa mashabiki katika duru ya Machakos.

Hata hivyo, alifafanua kuwa makanika, wadhamini, maafisa wa mashindano hayo na wanahabari watakubaliwa katika sehemu ya mashindano chini ya masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Watahitajika kuvalia barakoa wakati wote, kunawa mikono na kutokaribiana.

“Licha ya kuwa tunapenda mchezo huu, tutahakikisha kuwa usalama wa washiriki unadumishwa na hakuna shabiki ataruhusiwa,” alisema Kahumbura, ambaye pia ni mwenyekiti wa waandalizi wa Machakos Rally, Kenya Motor Sports Club.

You can share this post!

Sheria mpya za unywaji pombe Kiambu

FIFA yarefusha kipindi cha marufuku kwa vinara wake za...