• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Ingwe yapata pigo kusaini wachezaji baada ya FIFA kuipiga marufuku kutokana na deni la mamilioni kwa raia wa Rwanda

Ingwe yapata pigo kusaini wachezaji baada ya FIFA kuipiga marufuku kutokana na deni la mamilioni kwa raia wa Rwanda

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards imepigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kusaini wachezaji wapya.

Hii ni baada ya klabu hiyo kukosa kulipa aliyekuwa kiungo wake mkabaji Vincent Habamahoro malimbikizo ya mshahara wa Sh1.8 milioni.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya walijipata matatani dhidi Habamahoro aliyeondoka Ingwe mnamo Desemba 2019 akiwa anadaiwa klabu hiyo mshahara wa miezi minne. Alikuwa amejiunga na Ingwe mnamo Julai 21, 2019 kwa kandarasi ya miaka miwili akitokea nchini mwake Rwanda.

Ripoti zinasema kuwa Leopards ya kocha Patrick Aussems haikuweza kulipa fedha hizo kufikia siku ya mwisho ambayo ilikuwa imepewa. Sasa, haitaweza kuajiri wachezaji hadi mwisho wa msimu 2021-2022.

“Hii ni baada ya AFC Leopards kushindwa kutimiza siku ya mwisho ya kulipa Habamahoro fedha zake ndani ya siku 45 ilizokuwa imepewa na Fifa,” ripoti hizo zimesema Jumanne.

Mwezi Februari, ripori mbalimbali zilidai kuwa mabingwa wa Kenya Gor Mahia wanakabiliwa na tatizo sawa na hilo.

Gor, ambayo inanolewa na Mreno Carlos Vaz Pinto, inafaa kulipa winga Mtanzania Dickson Ambundo Sh1.3 milioni kwa kukiuka kandarasi.

Wanabenki wa KCB pia walionana uso kwa macho na Fifa baada ya kuamrishwa walipe beki kutoka Rwanda Gabriel Mugabo Sh1.8 milioni. Vilevile, Wazito ilipokea adhabu kali kutoka kwa Fifa mwaka 2020 ilipolazimishwa kulipa faini ya karibu Sh6 milioni kwa sababu sawa na zile za Leopards, KCB na Gor.

Ilikiuka kandarasi za mshambuliaji Paul Acquah (Ghana), beki Issofou Bourhana (Togo), kiungo Mansoor Safi Agu (Uganda), Augustine Out (Liberia) na Piscas Muhindo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo).

Ripoti zinasema kuwa Ingwe itaruhusiwa kusaini wachezaji mapema iwapo italipa deni la Habamahoro kabla ya mwisho wa 2021-2022.

  • Tags

You can share this post!

KWA KIFUPI: Janga la corona limetatiza pakubwa vita dhidi...

Kassim Majaliwa aendelea kuonyesha umahiri Zanzibar...