• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
Kivumbi na patashika Uingereza ikitifuana leo na Ujerumani katika hatua ya 16-bora kwenye Euro

Kivumbi na patashika Uingereza ikitifuana leo na Ujerumani katika hatua ya 16-bora kwenye Euro

Na MASHIRIKA

UINGEREZA watajaribu leo kuangusha Ujerumani kwa mara ya kwanza katika hatua ya mwondoano wa kipute cha haiba kubwa kwenye soka tangu 1966 ambapo Three Lions walipepeta Ujerumani 4-2 kwenye fainali ya Kombe la Dunia.

Mechi itakayokutanisha miamba hao wawili hii leo kwenye hatua ya 16-bora ya Euro itasakatiwa mbele ya mashabiki 40,000 uwanjani Wembley, London.

Mshindi wa gozi hilo atakutana na Uswidi au Ukraine kwenye robo-fainali itakayochezewa jijini Roma, Italia mnamo Julai 3, 2021.

Uingereza wamewahi kusonga mbele kwenye hatua ya mwondoano wa Euro mara moja pekee.

Hiyo ilikuwa 1996 ambapo waliwachabanga Uhispania kupitia mikwaju ya penalti kabla ya kuondolewa hatimaye na Ujerumani kwenye nusu-fainali kupitia penalti vilevile. Kichapo hicho ndicho cha pekee ambacho kimewahi kushuhudia Uingereza wakizidiwa maarifa kwenye pambano la haiba kubwa katika uwanja wao wa nyumbani.

Iwapo Ujerumani watapoteza, jambo ambalo hawajafanya katika jumla ya mechi saba zilizopita dhidi ya Uingereza uwanjani Wembley, basi itamaanisha kwamba mechi ya leo itakuwa ya mwisho kwa kocha Joachim Loew kusimamia kambini mwa mabingwa hao mara tatu wa Euro (1972, 1980, 1996) na wafalme mara nne wa dunia (1954, 1974, 1990, 2014).

Loew anatarajiwa kujiuzulu kambini mwa Ujerumani baada ya kampeni za Euro kukamilika na mikoba anayodhibiti kutwaliwa na kocha wa zamani wa Bayern Munich, Hansi Flick.

Uingereza walikamilisha kampeni zao za Kundi D kileleni baada ya kushinda Croatia 1-0, kuambulia sare dhidi ya Scotland na kupokeza Jamhuri ya Czech kichapo cha 1-0.

Kwa upande wao, Ujerumani ambao ni mabingwa mara tatu wa Euro walifungua kinyang’anyiro cha Kundi F kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Ufaransa kabla ya kucharaza Ureno 4-2 na kulazimishiwa na Hungary sare ya 2-2.

Walipokutana kwa mara ya mwisho kwenye Euro mnamo 1996, Ujerumani walipepeta Uingereza 6-5 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoshana nguvu kwa sare ya 1-1 kufikia mwisho wa dakika 120. Gareth Southgate ambaye kwa sasa ni kocha wa Uingereza, alipoteza penalti yake kwenye kipute hicho cha nusu-fainali.

Uingereza watajitosa ulingoni wakiwa na kiu ya kuendeleza rekodi nzuri ya kutofungwa hadi kufikia sasa kwenye Euro. Masogora hao wa Southgate pamoja na Italia ambao walitamalaki Kundi A, ndio wa pekee waliotinga hatua ya 16-bora mwaka huu bila ya wapinzani kutikisa nyavu zao.

Ingawa Uingereza hawajapoteza mechi yoyote kati ya tisa zilizopita, michuano minne ya hivi karibuni ambayo wameshinda imekamilika kwa bao 1-0. Kabla ya kuangusha Croatia na Jamhuri ya Czech kwenye Kundi D, walikuwa pia wamesajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Austria na Romania kirafiki.

Iwapo Uingereza watawalaza Ujerumani chini ya dakika 90, basi itakuwa mara ya kwanza kwa kikosi hicho kushinda gozi la hatua ya muondoano kwenye Euro katika muda wa kawaida.

Ujerumani almaarufu ‘Die Mannschaft’ wamefaulu kuingia nusu-fainali ya Euro mara tatu mfululizo tangu waanze kunolewa na Loew mnamo 2006. Walitinga hatua hiyo ya nne-bora mnamo 2008, 2012 na 2016.

Hadi walipokutana majuzi zaidi katika mechi ya kirafiki iliyokamilika kwa sare tasa mnamo 2017, Ujerumani waliwahi kuwakung’uta Uingereza 4-1 katika hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia mnamo 2010.

Rekodi ya Uingereza dhidi ya Ujerumani kwenye mechi za mwondoano:

1966: Fainali ya Kombe la Dunia: Uingereza 4-2 Ujerumani.

1970: Robo-fainali ya Kombe la Dunia: Uingereza 2-3 Ujerumani (baada ya muda wa ziada).

1990: Nusu-fainali ya Kombe la Dunia: Uingereza 3-4 Ujerumani (penalti baada ya sare ya 1-1).

1996: Nusu-fainali ya Euro: Uingereza 5-6 Ujerumani (penalti baada ya sare ya 1-1).

2010: Hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia: Uingereza 1-4 Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kocha Rafael Benitez atishiwa maisha anapojiandaa kuajiriwa...

Cecafa U23 yaahirishwa kutoka Julai 3 hadi Julai 17