• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Lionesses yaridhika na nambari 10 Olimpiki raga ikitamatika

Lionesses yaridhika na nambari 10 Olimpiki raga ikitamatika

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya raga ya wachezaji saba kila upande ya kinadada ya Kenya maarufu Lionesses, ilikamilisha kampeni yake ya Olimpiki 2020 katika nafasi ya 10 jijini Tokyo nchini Japan.

Vipusa wa kocha Felix Oloo walilemewa na Canada kwa alama 24-10 katika mechi ya kuamua nafasi ya tisa na 10 iliyosakatwa Julai 31.

Canada iliongoza 12-0 kupitia miguso ya Charity Williams na Bianca Farella na mkwaju wa Ghislaine Landry.

Lionesses ilipunguza mwanya huo kupitia mguso kutoka kwa Janet Okello kabla ya mapumziko. Farella alipachika mguso wake wa pili ulioweka Canada 17-5 juu kabla ya nahodha Landry kuongeza mguso na mkwaju kuimarisha uongozi huo hadi 24-5.

Diana Awino Ochieng’, ambaye aliingia kama kizibo cha Sinaida Aura katika kipindi cha pili, alifunga mguso wa pili na mwisho wa Kenya.

Lionesses, ambayo ilikamilisha Olimpiki 2016 katika nafasi ya 11 kati ya mataifa 12, ilipoteza mechi za Kundi A jijini Tokyo dhidi ya New Zealand 29-7, Urusi 35-12 na Uingereza 31-0 kabla ya kuduwaza Japan 21-17 katika nusu-fainali ya nambari tisa hadi 12.

Msimamo wa raga: Kinadada – New Zealand (washindi), Ufaransa, Fiji, Uingereza, Australia, Amerika, Uchina, Urusi, Canada, Kenya, Brazil, Japan; Wanaume – Fiji (washindi), New Zealand, Argentina, Uingereza, Afrika Kusini, Amerika, Australia, Canada, Kenya, Ireland, Japan, Korea Kusini.

  • Tags

You can share this post!

Covid: WHO yaelezea hofu ya virusi vipya vya Delta

Man-City waweka mezani Sh15.6 bilioni kwa ajili ya kiungo...