• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Man-City waweka mezani Sh15.6 bilioni kwa ajili ya kiungo Jack Grealish wa Aston Villa

Man-City waweka mezani Sh15.6 bilioni kwa ajili ya kiungo Jack Grealish wa Aston Villa

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City wamewasilisha ofa ya Sh15.6 bilioni kwa ajili ya kumsajili kiungo raia wa Uingereza, Jack Grealish ambaye kwa sasa ni nahodha wa Aston Villa.

Kocha Pep Guardiola wa Man-City amekuwa akihemea sogora huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa muda mrefu na amesisitiza kuwa kusajiliwa kwake kutamchochea pia nahodha wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane kutua uwanjani Etihad.

Man-City wako radhi kuweka mezani Sh15.6 bilioni nyingine kwa ajili ya maarifa ya Kane iwapo wataambulia pakavu katika juhudi zao za kumtwaa fowadi chipukizi wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, kumekuwepo na mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Man-City na Villa ili kupata mwafaka wa kumsajili Grealish ambaye anatarajiwa wiki ijayo kurejea katika kambi ya mazoezi ya Villa katika eneo la Bodymoor Heath, Uingereza.

Guardiola ameshikilia kuwa ujio wa Grealish utapiga jeki safu ya uvamizi na kuweka hai matumaini ya Man-City kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kuzidiwa ujanja na Chelsea kwenye fainali ya 2020-21 jijini Porto, Ureno.

Fedha ambazo Man-City wataweka mezani kwa minajili ya Grealish zitapita Sh12.4 bilioni zilizotolewa na Manchester United mnamo 2016 kwa ajili ya kumsajili upya kiungo Paul Pogba.

Fedha hizo zitakuwa kiasi cha juu zaidi kuwahi kutolewa na kikosi cha soka ya Uingereza kwa ajili ya mwanasoka yeyote.

Iwapo Man-City watamtwaa Grealish kwa Sh15.6 bilioni, basi atakuwa sogora ghali zaidi katika historia ya EPL. Ni wachezaji wanane pekee kufikia sasa ambao wamewahi kusajiliwa kwa zaidi ya Sh15 bilioni katika historia ya kabumbu.

Wanasoka waliosajiliwa kwa bei ya juu zaidi duniani:

Neymar (Barcelona hadi Paris St-Germain) – Sh26 bilioni mnamo 2017.

Kylian Mbappe (Monaco hadi Paris St-Germain) – Sh23 bilioni mnamo 2017.

Philippe Coutinho (Liverpool hadi Barcelona) – Sh19.8 bilioni mnamo 2018.

Ousmane Dembele (Borussia Dortmund hadi Barcelona) – Sh18.9 bilioni mnamo 2017.

Joao Felix (Benfica hadi Atletico Madrid) –

Sh15.8 bilioni mnamo 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Lionesses yaridhika na nambari 10 Olimpiki raga ikitamatika

Ahadi ya Omanyala kuzoa medali kwenye mbio za mita 100...