• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Nafuu Dortmund baada ya Haaland kupona kabla ya mechi dhidi ya Sevilla kwenye UEFA

Nafuu Dortmund baada ya Haaland kupona kabla ya mechi dhidi ya Sevilla kwenye UEFA

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund wamethibitisha kwamba fowadi chipukizi raia wa Norway, Erling Braut Haaland, atakuwa sehemu ya kikosi kitakachovaana leo Jumanne na Sevilla kwenye marudiano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Aidha, miamba hao wa soka ya Ujerumani wameungama kuwa kiungo Jadon Sancho atasalia mkekani kuuguza jeraha la paja ambalo pia litamkosesha mechi tatu zijazo za timu ya taifa ya Uingereza.

Haaland alifungia Dortmund mabao mawili mnamo Machi 6, 2021 katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) iliyoshuhudia chombo chao kikizamishwa na mabingwa watetezi Bayern Munich kwa magoli 4-2. Haaland aliondolewa uwanjani katika kipindi cha pili kwenye mchuano huo baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu.

“Haaland amepona kwa wakati na ataunga kikosi chetu cha kwanza dhidi ya Sevilla,” akasema kocha mshikilizi wa Dortmund, Edin Terzic.

Nyota huyo wa zamani wa RB Salzburg, alifungia Dortmund mabao mawili katika ushindi wa 3-2 waliousajili katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Februari 18, 2021.

Giovanni Reyna, Axel Witsel na Raphael Guerreiro ni wanasoka wengine wa haiba kubwa watakaokosa kuwa sehemu ya kikosi cha Dortmund.

Sevilla kwa upande wao wamepigwa jeki na marejeo ya kipa Yassine Bounou pamoja na beki mzoefu Jules Kounde ambao wamepona majeraha.

Chini ya kocha Julen Lopetegui, Sevilla wamepoteza mechi nne kati ya tano zilizopita katika mashindano yote. Washiriki hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) walipigwa 2-1 na Elche mnamo Jumamosi iliyopita (Machi 6, 2021), siku tatu baada ya Barcelona kuwabandua kwenye nusu-fainali za Copa del Rey kwa jumla ya mabao 3-2.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Ronaldo atakuwa tegemeo letu dhidi ya FC Porto –...

Ndoa ya BBI yaingia doa