• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Nusu-fainali ya Kenya Cup kati ya Kabras na Strathmore kuendelea baada ya kesi ya Quins dhidi ya Strathmore kutupwa nje

Nusu-fainali ya Kenya Cup kati ya Kabras na Strathmore kuendelea baada ya kesi ya Quins dhidi ya Strathmore kutupwa nje

Na GEOFFREY ANENE

MECHI za nusu-fainali za Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya) kati ya Kabras Sugar na Strathmore Leos na ile inayokutanisha KCB na Menengai Oilers zitaendelea jinsi zilivyopangwa Agosti 28 baada ya kesi ya Kenya Harlequin dhidi ya Strathmore kutupiliwa mbali Ijumaa.

Quins ilitaka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Strathmore waondolewe katika michuano hiyo kwa kukiuka sheria za mashindano.

Mwenyekiti wa Quins, Michael Wanjala aliwasilisha kesi mbele ya bodi ya rufaa ya Shirikisho la Raga Kenya (KRU) dhidi ya Strathmore mnamo Agosti 24. Alidai kuwa klabu hiyo kutoka mtaani Madaraka ilifaa kupokonywa alama mbili wala si kupewa idadi hiyo ya alama kwa kutocheza dhidi ya Mwamba.

“Kulingana na sheria zinazosimamia mashindano ya Kenya Cup, mechi ya Strathmore ya Agosti 21 ilifaa kuwa dhidi ya Mwamba, lakini waliamua kusafiri hadi ugani Nandi Bears katika kaunti ya Nandi kumenyana na Masinde Muliro kwa hivyo Mwamba walifaa kutunukiwa ushindi halafu Strathmore wapoteze mechi hiyo. Hata hivyo, mechi hiyo iliamuliwa kuwa sare huku ili isiyo halali ugani Nandi Bears ikatambuliwa,” alisema Wanjala alipowasilisha rufaa hiyo mbele ya Edward Rombo na Waiyaki Hinga.

Hapo Agosti 27, Wanjala alieleza Taifa Leo kuwa wamepokea uamuzi wa kesi hiyo. “Rufaa yetu imetupwa nje. Tunasikitika kwa sababu tulihisi kuwa masharti mengi na taratibu zilivunjwa, lakini tunaheshimu uamuzi huo. Tunatumai kuwa kesi hii itakuwa funzo kwa KRU kufuata masharti na taratibu zinazosimamia mchezo wa raga,” alitanguliza afisa huyo.

Sababu zilizotolewa kwa kutupiliwa mbali kwa rufaa hiyo, Wanjala alisema, ni kuwa bodi hiyo ilihisi kuwa KRU ilifuata sheria katika kuamua mechi kati ya Mwamba na Strathmore ni sare na pia ilidumisha matokeo ya mchuano huo.

“Katika rufaa yetu, tulisema kuwa sheria hazikufuatwa kwa hivyo mchuano huo ulifaa ufutiliwa mbali,” alisema Wanjala ambaye timu yake ya Quins ilikamilisha msimu wa kawaida katika nafasi ya tano kwa alama 25, mbili nyuma ya nambari nne Strathmore.

Wanasukari wa Kabras, ambao wataalika Strathmore ugani Nandi Bears, walimaliza juu ya jedwali katika msimu wa kawaida kwa jumla ya alama 49. Kabras inanolewa na Dominique Habimana naye Louis Kisia anashikilia usukani Strathmore.

Nusu-fainali kati ya KCB na Oilers itapigiwa ugani KCB Ruaraka jijini Nairobi. Timu hizo zilimaliza msimu wa kawaida katika nafasi ya pili na tatu kwa alama 44 na 30, mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Raila amtaka Mutyambai asafishe polisi kuondoa uozo

Chokoraa 15 washtakiwa kwa kutovalia barakoa