• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Okutoyi afika Casablanca salama kukuza talanta yake ya tenisi zaidi

Okutoyi afika Casablanca salama kukuza talanta yake ya tenisi zaidi

Na GEOFFREY ANENE

MWANATENISI Angella Okutoyi ametua salama salmini nchini Morocco ambako atakita kambi kwenye kituo cha kukuza talanta cha Shirikisho la Tenisi Duniani (ITF) mjinini Casablanca.

Bingwa huyo wa Kenya Open 2018, ambaye majuzi alibeba mataji ya mashindano ya daraja ya nne ya chipukizi (J4 Nairobi I & II) jijini Nairobi na kuruka kutoka nafasi ya 186 duniani hadi 127, aliondoka nchini Jumatano usiku na kuwasili Alhamisi alasiri.

Akiwa Casablanca, Okutoyi atapata mafunzo ya hali ya juu ya tenisi na kushiriki mashindano ya daraja ya kwanza na pili (J1&2), lakini nje ya taifa hilo la kaskazini magharibi mwa Afrika.

“Lengo kubwa ni kuhakikisha anafaulu kushiriki mashindano ya kifahari ya chipukizi (Junior Grand Slam) kuanzia mwezi Mei kwenye French Open. Lazima aingia mduara wa 100-bora ndiposa aweze kushiriki mashindano ya Junior Grand Slam,” alisema kocha wake Francis Rogoi katika mahojiano ya awali.

Okutoyi, ambaye alisherehekea kufikisha umri wake 17 hapo Januari 29, ni Mkenya wa pili kupitia kituo cha kukuza talanta cha Casablanca baada ya Ismael Changawa Ruwa Mzai,24.

You can share this post!

Mvua ya mabao Everton wakidengua Tottenham kwenye raundi ya...

Mudavadi, Kalonzo wamtaka Raila akae kando 2022