• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Phil Foden kuwania mataji mawili kwenye tuzo za PFA ambazo zimetamalakiwa na wanasoka wa Manchester City

Phil Foden kuwania mataji mawili kwenye tuzo za PFA ambazo zimetamalakiwa na wanasoka wa Manchester City

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Manchester City, Phil Foden, ameteuliwa kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka na lile la Chipukizi Bora wa Mwaka kwenye tuzo za Chama cha Wanasoka Wataalamu (PFA).

Orodha ya wanasoka wanaowania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka limetamalakiwa na masogora wa Man-City wakiwemo viungo Ilkay Gundogan na Kevin de Bruyne pamoja na beki Ruben Dias. Orodha hiyo inakamilishwa na Bruno Fernandes wa Manchester United na Harry Kane wa Tottenham Hotspur.

Washindi wa tuzo hizo watatangazwa mnamo Jumapili ya Juni 6, 2021.

Foden, 21, alichezea Man-City mara 50 kwenye kampeni zote za msimu huu wa 2020-21 na kusaidia waajiri wake hao kutia kapuni taji la Carabao Cup na ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Tangu awajibishwe na timu ya taifa ya Uingereza kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 2021, Foden amekuwa akiridhisha ndani ya jezi za kikosi hicho kiasi cha kocha Gareth Southgate kumjumuisha katika kikosi atakachokitegemea kwenye fainali zijazo za Euro.

Tuzo ya PFA kwa Chipukizi Bora wa Mwaka hutolewa kwa wanasoka wasiozidi umri wa miaka 23 japo pia wana uhuru wa kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka.

Ni wanasoka watatu pekee ambao wamewahi kunyanyua mataji hayo mawili ya PFA kwa msimu mmoja tangu tuzo hizo zianzishwe mnamo 1973-74. Hao ni Andy Gray mnamo 1976-77, Cristiano Ronaldo mnamo 2006-07 na Gareth Bale mnamo 2012-13.

Bukayo Saka wa Arsenal, Declan Rice wa West Ham United, Mason Greenwood wa Manchester United, Mason Mount wa Chelsea na Trent Alexander-Arnold wa Liverpool ni masogora wengine wanaowania taji la Chipukizi Bora wa Mwaka.

Wanasoka watatu wa Chelsea – Sam Kerr, Ann-Katrin Berger na Fran Kirby ni miongoni mwa masogora wanaowania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA kwa upande wa wanawake.

Beki raia wa Ureno, Dias, alijiunga na Man-City mnamo Septemba 2020 baada ya kukatiza uhusiano wake na Benfica ya Ligi Kuu ya Ureno. Alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020-21 na Chama cha Wanahabari wa Soka (FWA) mnamo Mei 2021 na ni miongoni mwa wachezaji ambao wameteuliwa kuwania taji la Mchezaji Bora wa Msimu wa 2020-21 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mnamo 2019-20, De Bruyne alitwaa taji la Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA huku beki Alexander-Arnold wa Liverpool akitwaa tuzo ya Chipukizi Bora wa Mwaka.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chelsea na Man-City watamalaki orodha ya wawaniaji wa tuzo...

Muller na Hummels wachezea Ujerumani kwa mara ya kwanza...