• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Pwani ina wanariadha wa mbio, kinachohitajika ni mikakati ya kukuza talanta

Pwani ina wanariadha wa mbio, kinachohitajika ni mikakati ya kukuza talanta

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KUNA wanaoamini kuwa katika eneo la Pwani kuna wanariadha wengi wenye vipaji vya mbio kiasi kuwa wengineo huwa wamefichika huko mashinani.

Kuna wanariadha chipukizi kwenye shule za msingi na upili na hasa Kaunti ya Taita Taveta ambao wakiangaziwa na kupatiwa fursa ya kuinua vuipaji vyao, wanaweza kufika mbali sawa na alivyo mwanariadha wa kaunti hiyo, Panuel Mkungo.

Hivi sasa, Mkungo anaishi Amerika ambakio anapata fursa ya kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa na hasa yale ya Mbio za Barabarani na Half Marathon.

Japo katika kaunti hiyo hapajatokea mwanariadha msichana aliyepiga hatua sawa na ile Mkungo amefikia, lakini wako ambao wanaonyesha dalili kama watalelewa vizuri na kusaidiwa, wataweza kutambulika kwa muda mfupi ujao.

Wakati wa Mbio za Nyika za jimbo la Pwani zilizofanyika uwanja wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi, kulikuweko na wakimbiaji chipukizi watatu, wasichana wawili na mvulana mmoja wanaotoka ukoo mmoja na ambao walionyesha kuwa wana vipaji vya mchezo wa riadha.

Maria Shali Mwashigadi, msichana wa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi ya Shagha, alishangaza mashabiki wa kiasi wakiwemo maofisa wa tawi la Pwani wa Chama cha Riadha (AK) alipoibuka mshindi wa mbio za kilomita 5 kwa wasichana wa umri chini ya miaka 18.

Maria aliye na umri wa miaka 12 aliibuka mshindi katika mbio hizo kwa kutumia dakika 23 nukta 14.16 akifuatiwa na dadake mkubwa Agnes Mwashigadi, mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Shule ya Upili ya Kitumbi High aliye na umri wa miaka 16 aliyetumia dakika 23:54.22.

Pacha wake Agnes, Samuel Mwashigadi ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Nane wa shule ya Shagha Primary alimaliza nafasi ya nne katika mbio za wavulana wa umri chini ya miaka 18 za kilomita 6 alipotumia dakika 18:44.46.

Maria anasema anataka kuwa mwanariadha wa kimataifa na kuwakilisha taifa lake kwenye mashindano na michezo ya kimataifa.

“Ninapoona wakimbiaji wa Kenya, huwa na hamu na mimi nikiwa mkubwa nitajike kote duniani,” amesema Maria.

Maria Mwashigadi (kati) akipokea cheti chake cha kumaliza mshindi wa kitengo cha wasichana wa umri chini ya miaka 18 huku dadake Agnes (kulia) aliyemaliza nafasi ya pili akishuhudia. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Agnes anasema ana huzuni kubwa kuwa hapati fursa ya kufanya mazoezi kwa sababu shule anayosoma haifanyi huo mchezo.

“Ningeomba nitafutie chuo ambacho nitapata mafunzi ya riadha kwani nina uhakika ninaweza kufanikiwa kuiwakilisha nchi yangu,” akasema.

Agnes anasema ana matumaini kilio chake cha kutaka kupata sehemu ambayo atapata mafunzo ya kukimbia kitaitikiwa kwani ana uhakika ataweza kuwa mmoja wa wakimbiaji mahiri.

“Nataka nitajike kama alivyo nahodha wetu Panuel Mkungo, nikipata usaidizi, nitafanikiwa,” akasema.

Agnes amesema anaomba adhaminiwe kwenye shule ambayo inafanya michezo ili kipaji chake cha mbio apate kukihifadhi na kuendelea nacho.

“Shule nisomayo hatufanyi michezo wala mazoezi,” akasema.

Samuel Mwashigadi anasema kuwa amefurahi kufanikiwa kuwakilisha Pwani kwenye mbio za kitaifa japo amemaliza nafasi ya nne lakini akaahidi mara nyingine kufanya vizuri zaidi.

“Natamani tusaidiwe tuendeleze vipaji vyetu,” akasema.

Wana familia hao watatu ya Mwashigadi, wamefuzu kwenga kushiriki kwenye Mbio za Nyika za Kitaifa zitakazofanyika huko Ngong Racecourse jijini Nairobi siku ya Jumamosi, Februari 13.

La kusikitisha zaidi ni kuwa familia hiyo ya wakimbiaji hawa watatu ikiwa pamoja na kaka yao Sheltel Mwachofi, mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Funju Secondary, inaishi katika hali ya umasikini katika kijiji cha Nyache. lakini Sheltel hakujitosa kwenye mchezo wowote.

Watoto hao wanaishi na kulelewa na babu yao Paulo Mlewa na nyanya yao Agnes Samba. Mlewa alifahamisha kuwa wajukuu zake hao waliwapoteza wazazi wao mwaka 2008 baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu.

“Wajukuu zangu hawa wanapenda sana kukimbia na kila asubuhi wanapokwenda shule wanakimbia na wakirudi wanarudi kwa kukimbia, wanapenda sana mchezo wa mbio,” akasema Mlewa.

  • Tags

You can share this post!

Bayern wana kiu ya kutwaa Kombe la Dunia kwa Klabu nchini...

Walioteuliwa kuwania wadhifa wa Jaji Mkuu watangazwa