• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
South C Ladies: Soko inavyowasisimua mabinti wa mitaani

South C Ladies: Soko inavyowasisimua mabinti wa mitaani

NA PATRICK KILAVUKA

Timu ya akina dada ya South C Ladies Academy iliasisiwa kutokana na nia ya mabinti hao kutaka kujua jinsi ya kusakata boli wakati walipokuwa wakiona madume wa timu hiyo wakipiga gozi uwanjani CID, South C kila mara.

Akina dada hao waliazimia kwamba litakuwa jambo jema iwapo wanaweza kukuja pamoja na kusakata boli na mwaka 2015, walianza kujituma kuvikuza vipaji vyao vya kabumbu.

Isitoshe, wazo lao lilikuwa na mashiko kwa mkufunzi Abudallah Munyua na naibu wake Aymam Raba na vipawa vyao vikawa na msingi mwema kwa kufinyangwa.

Wanasoka hawa wanatoka sehemu mbalimbali za jiji kujifua mazoezini uwanjani CID. Pembe wanazotoka ni Westlands, Hurlingham, Eastleigh, Karen na South B.

Kulingana na naibu mkufunzi Raba, wachezaji hao hukutana Jumamosi na Jumapili kujinoa kwa sababu miongoni mwao kuna wanafunzi wa shule mbalimbali na wengine hufanya kazi na hupata nafasi tu wikendi kuhudhuria mazoezi au kupiga mechi za kujitia makali.

Kikosi cha akina dada cha South C Academy kisherekea baada ya kufunga bao dhidi ya wapinzani Otto Benecker. Picha/Patrick Kilavuka

Kuanzisha kwa timu hii kumewafaa wachezaji hao kwani kumeepusha na maovu mengi ya kijamii ambayo huwakabili wasichana wa umri wao na wanafurahia sana kutumia wakati wao kutimiza ndoto zao za kusakata mpira.

Msaidizi wa kocha huyo anasema wengi wa wanadimba hao hawakuwa wametambua talanta zao vyema na hakuwa wamejua lolote katika kandanda lakini ari yao imewapelekea kujifunza mengi ya kuwafikishwa kwenye ufanisi na kunawiri.

“Wamejifunzwa kudhibiti boli, pasi za uhakika, ujuzi, kasi ya kucheza na mazoezi ya viungo ambayo yamewaongezea usuli, ” anasema kocha huyo na kukariri kwamba timu itaendelea kuandaliwa kupitia vipute pia.

Tayari wana mataji mawili kabatini mwao yakiwa lile la Oshwal Cup Ladies 2019 na Mwakilishi wa Wadi ya South C, mwaka huo.

Kikosi cha akina dada cha South C Academy kikicheza dhidi ya Otto Benecker uwanjani Kihumbuini, Kangemi katika kinganganyiro cha Westlands Soka Association.Picha/Patrick Kilavuka

Wakati huu, kocha Raba anasema timu inapiga hatua kujengwa japo corona iliathiri mazoezi awali.

“Timu imeanza kuinuka na juzi ilipata fursa ya kujitosa katika kipute cha Westlands Soka Association (Akina dada) ingawa ilisaza kiputeni baada ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Otto Benecker na kuwabwaga 2-1 uwanjani Kihumbuini,”asema mkufunzi Raba.

Kwa muda timu imekuwa hai katika ulimwengu wa soka, imemtoa mchezaji Oneza ambaye alijiinga na akademia ya Manchester United- akina dada.

Wanakikosi wanajumuisha Zahra Mohammed, Muniba Abdikarim, Salwa Ali, Jenny Kahamba, Esther Chege, Fatma Mohammed, Maggy Kahamba, Area Feisaz, Ifrah Abdullah, Valerie Danvers, Nasra Hassan, Susan Kerubo, Rhianna Firoz, Carol Wambugu na Sam Mohammed.

You can share this post!

KENNEDY OSORE: Soka inavyokuza maadili katika jamii

BBI kuangushwa katika kura ya maamuzi – Utafiti