• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Tottenham wana matatizo mengi ambayo siwezi kutatua – Mourinho

Tottenham wana matatizo mengi ambayo siwezi kutatua – Mourinho

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba kikosi chake cha Tottenham Hotspur kina matatizo mengi ambayo yeye mwenyewe hawezi kuyatatua.

Hata hivyo, anaungama kuwa kichapo cha 2-1 walichopokezwa na West Ham United katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili hakijasambaratisha maazimio ya vijana wake kwenye kampeni za muhula huu.

Kichapo kutoka kwa West Ham kilikuwa cha tano kwa Tottenham kupokea kutokana na mechi sita zilizopita. Matokeo hayo ya Tottenham dhidi ya West Ham yalisaza kikosi cha Mourinho katika nafasi ya tisa kwa alama 36 sawa na Aston Villa waliochabangwa na Leicester City 2-1 katika mechi nyingine ya EPL mnamo Jumapili.

Mabao ya West Ham dhidi ya Tottenham yalifumwa wavuni kupitia Michail Antonio na Jesse Lingard anayechezea kikosi hicho cha kocha David Moyes kwa mkopo kutoka Manchester United. Tottenham walifungiwa bao lao na Lucas Moura.

“Siwezi kusema kwamba tunapitia changamoto ambazo zinaweza kutusambaratisha. Lakini tunapitia kipindi kigumu ikizingatiwa ubovu wa matokeo ambayo tunapitia kwa sasa. Tunapoteza idadi kubwa ya michuano,” akasema kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United.

Kwa upande wao, West Ham walipaa hadi nafasi ya nne kwa alama 45, nne pekee nyuma ya Leicester na Man-United. Ni pengo la pointi mbili ndilo linawatenganisha West Ham na nambari tano Chelsea.

Kabla ya mechi kati ya West Ham na Tottenham, magazeti mengi nchini Uingereza yalidai kwamba Mourinho angejiweka katika hatari zaidi ya kupigwa kalamu na waajiri wake iwapo angeshindwa kusajili ushindi dhidi ya West Ham uwanjani London.

Licha ya mbinu zake za ukufunzi kukosolewa pakubwa na mashabiki katika siku za hivi karibuni, Mourinho alisisitiza kwamba “benchi ya kiufundi ya Tottenham kwa sasa ndiyo bora zaidi duniani”.

“Tottenham inajivunia wakufunzi wazoefu na bora zaidi duniani. Kwa muda mrefu sasa, tumekuwa na matatizo ambayo kwa mujibu wangu, siwezi kuyatatua kikamilifu kama kocha,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Ureno.

Mourinho anaamini kwamba itakuwa vigumu kwa Tottenham kufuzu moja kwa moja kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, na njia ya pekee katika kuweka hai matazamio hayo ni kutia kapuni taji la Europa League muhula huu.

Ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na Tottenham dhidi ua Wolfsberger ya Austria kwenye mkondo wa kwanza wa Europa League jijini Budapest unawaweka pazuri kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya kipute hicho kadri wanavyojiandaa kwa marudiano mnamo Alhamisi ya Februari 25.

“Matumaini yetu ya kunyanyua ufalme wa Europa League yangali hai. Hiyo ndiyo fursa ya pekee ya kutuwezesha kunogesha kivumbi cha UEFA msimu ujao,” akaongeza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Shujaa yaridhika nambari mbili Madrid 7s Lionesses ikivuta...

MKU, WEF waingia katika mkataba wa kuinua wanawake kiuchumi