• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Tottenham wasema hawana haraka ya kujaza pengo la kocha Mourinho

Tottenham wasema hawana haraka ya kujaza pengo la kocha Mourinho

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamekiri kwamba hawana haraka ya kutafuta kocha atakayerithi mikoba ambayo mkufunzi raia wa Ureno, Jose Mourinho alipokonywa kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Aprili 19, 2021.

Kumekuwepo na tetesi tele kuhusu kocha wa kujaza pengo hilo huku Julian Nagelsmann wa RB Leipzig, Erik ten Hag wa Ajax na Brendan Rodgers wa Leicester City wakiwa miongoni mwa wakufunzi waliopigiwa upatu wa kutwaa mikoba ya Spurs.

Hata hivyo, Nageslmann amekubali kujiunga na Bayern Munich kuwa mrithi wa Hansi Flick kuanzia mwanzo wa msimu ujao huku Ten Hag, 51, akitia saini mkataba mpya utakaomdumisha sasa kambini mwa Ajax ya Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) hadi mwisho wa Juni 2023.

Rodgers naye ambaye amewahi kuwanoa Liverpool na Celtic, amefichua maazimio ya kuendelea kuhudumu ugani King Power huku kikosi chake kikipigania sasa nafasi ya kukamilisha kampeni ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Matukio hayo yameibua tetesi kwamba Spurs wanahangaika pakubwa katika juhudi za kusaka kocha mpya – madai ambayo mwenyekiti Daniel Levy amekanusha.

“Usimamizi utachukua muda kabla ya kuanza mchakato wa kutafuta kocha mpya. Isitoshe, bado hatujaanza shughuli ya kutathmini kuhusu mkufunzi anayefaa zaidi kati ya wengi wanaopatikana kwa sasa,” akasema kinara huyo.

Chombo cha Spurs kwa sasa kinaongozwa na kocha Ryan Mason aliyewahi kuwa mchezaji wa kikosi hicho kilichompokeza mikoba ya akademia mnamo 2018.

Ilivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mason, 29, ataendelea kuwa kocha mshikilizi wa Spurs kwa kipindi kirefu zaidi huku akisaidiana na Chris Powell, Nigel Gibbs, Ledley King na Michel Vorm ambaye ni kocha wa makipa.

Kufikia sasa, Spurs wamejizolea alama 53 kutokana na mechi 33 zilizopita na wanajiandaa kuvaana kesho na Sheffield United katika mchuano watakaopania kuwapa jukwaa la kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa soka ya bara Ulaya muhula ujao. Ni pengo la alama 10 ndilo linawatenganisha Spurs na nambari tatu Leicester.

Akihojiwa na Time Magazine nchini Uingereza mnamo Ijumaa, Mourinho alisema kwamba itamchukua muda mrefu kabla arejee ugani kuendeleza taaluma yake ya ukufunzi.

Kocha huyo aliyetimuliwa mwenye umri wa miaka 58 aliyetimuliwa na Spurs baada ya miezi 17 pekee, sasa atakuwa mchambuzi wa mechi wakati wa fainali za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Mourinho amewahi pia kutia makali vikosi vya Chelsea, Manchester United, Inter Milan, Real Madrid na FC Porto. Alipoteza jumla ya mechi 10 akidhibiti chombo cha Spurs msimu huu , hii ikiwa mara ya kwanza katika historia yake ya ukufunzi kupoteza idadi kubwa zaidi ya michuano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uhuru aondoa amri ya kutoingia na kutoka kaunti tano...

Sagan Tosu na Vissel Kobe washinda ligini Japan bila huduma...