• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Ufaransa wapepeta Wales 3-0 kirafiki

Ufaransa wapepeta Wales 3-0 kirafiki

Na MASHIRIKA

KADI nyekundu ambayo mchezaji Neco Williams alionyeshwa katika kipindi cha kwanza iliweka timu ya taifa ya Wales katika ulazima wa kucheza kwa zaidi ya dakika 60 ikiwa na wanasoka 10 pekee uwanjani katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ufaransa mnamo Jumatano usiku mjini Nice.

Ufaransa walisajili ushindi wa 3-0 katika mchuano huo uliokuwa ukitumiwa pia na Wales kujiandaa kwa fainali zijazo za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Williams ambaye ni beki wa Liverpool alifurushwa uwanjani katika dakika ya 25 baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alinawa mpira kimakusudi ili kuzuia mpira uliokuwa umeelekezwa kimiani mwao na fowadi wa Real Madrid, Karim Benzema.

Benzema aliyekuwa akiwajibikia Ufaransa kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita, alishuhudia mkwaju wake wa penalti ukipanguliwa na kipa Danny Ward aliyemnyima pia kiungo Adrien Rabiot nafasi kadhaa za wazi hadi wakati ambapo alizidiwa ujanja na Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain (PSG) katika dakika ya 34.

Mabao mengine ya Ufaransa yalifumwa wavuni na Antoine Griezmann na Ousmane Dembele katika dakika za 47 na 79 mtawalia.

Chini ya kocha mshikilizi Robert Page, Wales wameratibiwa kuanza kampeni zao za Euro dhidi ya Uswisi mnamo Juni 12. Kikosi hicho kinachojivunia huduma za wanasoka Gareth Bale na Aaron Ramsey, kilitinga nusu-fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AKILIMALI: Jinsi mfugaji anavyoweza kukabili kero ya...

Uingereza wakomoa Austria na kujiweka sawa kwa kampeni za...