• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Vipusa wa Uingereza kuvaana na Northern Ireland mnamo Oktoba katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia ugani Wembley

Vipusa wa Uingereza kuvaana na Northern Ireland mnamo Oktoba katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia ugani Wembley

Na MASHIRIKA

UINGEREZA watacheza na Northern Ireland katika mchuano wa kufuzu kwa Kombe la Dunia mnamo Oktoba 2021, hiyo ikiwa mara ya kwanza kwa vipusa hao kuchezea mechi ya haiba kubwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Wembley tangu ufunguliwe upya mnamo 2007.

Uingereza almaarufu Lionesses walicheza na Ujerumani katika mechi mbili za kirafiki uwanjani Wembley mnamo Novemba 2014 na Novemba 2019.

Tiketi za kuhudhuria mchuano kati ya Uingereza na Northern Ireland zitaanza kuuzwa mnamo Agosti 5, 2021.

Mechi ya kirafiki iliyoshuhudia Ujerumani wakizaba Uingereza 2-1 mnamo 2019 iliweka rekodi ya kuwa mchuano wa wanawake uliohudhuriwa na mashabiki wengi zaidi wa nyumbani katika ardhi ya Uingereza. Mechi hiyo ilivutia mashabiki 77,768.

Mechi ya soka ya wanawake iliyowahi kuhudhuriwa na idadi kubwa zaidi ya mashabiki nchini Uingereza ni ile iliyoshuhudia vipusa wa Amerika wakiwapiga Japan kwenye fainali ya Olimpiki za London mnamo 2012. Gozi hilo lilivutia mashabiki 80,023.

Northern Ireland walisafiri hadi uwanjani St George’s Park mnamo Februari 2021 kuvaana na Uingereza kirafiki na wenyeji wakasajili ushindi wa 6-0.

Timu hizo huenda zikakutana tena kwenye fainali za Euro mnamo Julai 2022 katika mchuano ambao utakuwa wa kwanza wa haiba kubwa zaidi kwa warembo wa Northern Ireland kunogesha.

Uingereza wataanza kampeni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo Septemba 17, 2021 dhidi ya Macedonia Kaskazini huku Northern Ireland wakichuana na Luxembourg.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Hofu idadi ya maambukizi ya corona ikipanda tena nchini

Wanawake sasa walilia usalama katika kampeni