• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
World Rugby yapongeza Mkenya Humphrey Kayange kuingia kamati ya IOC

World Rugby yapongeza Mkenya Humphrey Kayange kuingia kamati ya IOC

Na GEOFFREY ANENE

MWENYEKITI wa Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby), Sir Bill Beaumont amepongeza nyota wa zamani wa Kenya Shujaa, Humphrey Kayange mnamo Agosti 10.

Hii ni baada ya Kayange kuchaguliwa kuwa mwanakamati wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kufuatia kuteuliwa kwake na rais wa IOC Thomas Bach kutumikia Kitengo cha Wanamichezo.

Kayange, ambaye ni mwenyekiti wa Kitengo cha Wanamichezo kwenye Kamati ya Kitaifa ya Kenya (NOC-K), aliapishwa rasmi katika wadhifa wake katika mkutano wa IOC jijini Tokyo nchini Japan. Yeye ni mwanaolimpiki wa kwanza kutoka raga kuteuliwa katika mojawapo ya vitengo hivyo muhimu vya IOC vya kutoa uamuzi.

Kayange, 39, ambaye alipeperusha bendera ya Kenya kwenye Raga za Dunia kwa zaidi ya miaka 10, alikuwa katika timu iliyofaulu kushawishi IOC kurejesha raga kwenye Olimpiki mwaka 2009.

Pia, alikuwa katika kikosi cha Shujaa kilichoshiriki makala ya kwanza ya raga ya wachezaji saba kila upande kwenye Olimpiki mwaka 2016 jijini Rio de Janeiro nchini Brazil.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Mwamba aliwahi kutiwa katika orodha ya wawanizi wa tuzo ya mchezaji bora wa Raga za Dunia mwaka 2009 na 2013.

Ugombea uchaguzi wa Kayange ulilenga kuwapa uwakilishi wa nguvu wanamichezo kutoka mataifa madogo ama yanayokuwa ambayo yanapitia changamoto za kipekee. Pia, alilenga kupigania usawa katika michezo.

“Kwa niaba ya familia ya raga duniani, napongeza Humphrey kwa kuchaguliwa kwake kama mwanakamati wa IOC na kuteuliwa kutumia Kitengo cha Wanamichezo,” alisema Beaumont.

“Humphrey aliwakilisha vyema taifa lake na michezo uwanjani kwa zaidi ya miaka 10, alikuwa muhimu katika raga kurejea Olimpiki na amewasilisha maoni ya wanamichezo vyema kwa njia ya Kikenya, Kiafrika na raga.

“Kuteuliwa kwa Humphrey ni sahihi tosha kwa raga. Tutampa usaidizi wote anaohitaji kufanyia wanamichezo wote kazi wakiwemo wanaraga, ndani ya muungano wa Olimpiki.”

Kauli ya Beaumont iliungwa mkono na mwanakamati wa World Rugby, Angela Ruggiero, ambaye aliwahi kuhudumu kama mwanakamati wa IOC, Bodi Kuu ya kamati hiyo pamoja na mwenyekiti wa Kitengo cha Wanamichezo.

Kayange anajiunga na kitengo hicho kipya cha wanamichezo kinachoongozwa na Emma Terho kutoka Finland, ambaye amejiunga na Bodi Kuu ya IOC.

Shujaa wa mpira wa vikapu wa Uhispania Pau Gasol, muogeleaji Mwitaliano Federica Pellegrini, Mjapani Yuki Ota anaecheza mchezo wa “fencing” na muendeshaji wa baiskeli Maja Martyna Wloszczowska, pia ni wanakamati wa IOC baada ya kuchaguliwa kutumikia Kamati ya wanamiochezo ya IOC.

You can share this post!

Hakimu ashuku ipo njama kuchelewesha kesi ya ufisadi dhidi...

Danny Ings abanduka Southampton na kutua Aston Villa