• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Zidane atupilia mbali madai kwamba atajiengua kambini mwa Real Madrid mwisho wa msimu huu

Zidane atupilia mbali madai kwamba atajiengua kambini mwa Real Madrid mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

KOCHA Zinedine Zidane amekana madai kwamba amewaambia wanasoka wake wa Real Madrid kwamba ataagana na kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Vyombo vingi vya habari nchini Uhispania vilidai kwamba mkufunzi huyo raia wa Ufaransa alikuwa amewafichulia baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kuhusu mipango ya kuondoka uwanjani Santiago Bernabeu wiki moja iliyopita baada ya Real kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Sevilla ligini.

Chini ya Zidane, Real walisajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao mnamo Jumampili na kufanya mshindi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu kujulikana siku ya mwisho ya kampeni.

“Ningewaambiaje wachezaji kwamba ninapanga kuondoka? Ninafahamu mwajiri wangu. Kwa sasa macho yetu yameelekezwa kwa ubingwa wa La Liga na tunafanya kila liwezekanalo kuhifadhi taji hilo. Tutajua kitakachofanyika mwisho wa msimu,” akatanguliza Zidane.

“Watu nje ya kikosi wana uwezo wa kusema chochote wanachokipenda lakini siwezi kabisa kuwaelezea wachezaji wangu kwamba naondoka. Hilo ni jambo la kufichuliwa kwa wasimamizi wa kikosi,” akasema mchezaji huyo wa zamani wa Real na Juventus.

Real kwa sasa wanakamata nafasi ya pili jedwalini kwa alama 81, mbili nyuma ya viongozi Atletico waliolazimika kutoka nyuma na kupokeza Osasuna kichapo cha 2-1 mnamo Jumapili.

Chini ya Zidane, Real wameratibiwa kuvaana na Villarreal katika mechi yao ijayo ligini uwanjani Bernabeu. Miamba hao watafaulu kuhifadhi ufalme wa La Liga iwapo watashinda Villarreal nayo Atletico ya kocha Diego Simeone iambulie sare au ipigwe na Real Valladolid ugenini.

Zidane, 48, anahudumu kambini mwa Real kwa awamu ya pili baada ya kuongoza waajiri wake kutia kapuni mataji matatu mfululizo ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kati ya 2016 na 2018.

Kandarasi ya sasa kati ya Zidane na Real inatazamiwa kutamatika mnamo Juni 2022.

“Kuna wakati ambapo mabadiliko ni bora kwa kila mtu. Unaweza kutia saini mkataba wa miaka 10 na kikosi fulani na ukateua kutamatisha baada ya miezi 12. Pia unaweza kusaini kandarasi ya mwaka mmoja na ukaishia kuhudumu mahali kwa miaka mingi. Uteuzi huwa ni wa mtu binafsi,” akasema Zidane mnamo Jumamosi.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, tangazo la Zidane ni zao la hofu ya kutimuliwa na Real ambao walibanduliwa na Chelsea kwenye nusu-fainali za UEFA msimu huu huku matumaini yao ya kuhifadhi ufalme wa La Liga yakididimia.

Zidane alirejea ugani Santiago Bernabeu kudhibiti mikoba ya Real mwishoni mwa msimu wa 2018-19 baada ya matokeo ya kikosi hicho kushuka chini ya wakufunzi wawili – Julen Lopetegui na Santiago Solari walioaminiwa fursa za kurithi mikoba aliyoacha.

Juventus wanahusishwa pakubwa na uwezekano wa kumsajili Zidane ikizingatiwa kwamba miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) huenda wakampiga kalamu mkufunzi Andrea Pirlo baada ya matokeo duni msimu huu. Zidane aliwahi kuwa mchezaji wa Juventus na akawa kipenzi cha mashabiki wengi jijini Turin, Italia.

Hata hivyo, itamlazimu kukubali mshahara uliopunguzwa kwa asilimia kubwa kutoka ule wa Sh1.7 bilioni ambao kwa sasa anapokezwa na Real ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la UEFA.

Wakufunzi Raul Gonzalez, Massimiliano Allegri na Joachim Loew ndio wanahusishwa pakubwa na uwezekano wa kutwaa mikoba ya Real iwapo Zidane atajiengua mwishoni mwa msimu huu.

Loew anatazamiwa kuagana rasmi na timu ya taifa ya Ujerumani mwishoni mwa fainali za Euro mwaka huu na nafasi yake kambini mwa mabingwa hao wa zamani wa dunia inahusishwa pakubwa na kocha wa sasa wa Bayern Munich, Flick Hansi atakayejiengua kambini mwa miamba hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mwishoni mwa msimu huu.

Kwa upande wake, Allegri hajawahi kuajiriwa na kikosi chochote tangu atimuliwe na Juventus mnamo Mei 2019 naye Gonzalez, 43, kwa sasa anadhibiti mikoba ya chipukizi wa Real (Castilla).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

HAWA LEICESTER: Bao la Youri Tielemans kwenye fainali...

Serikali kuwasilisha rufaa kortini leo