• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Hatuogopi mswada wa kumtimua Ruto serikalini – Kositany

Hatuogopi mswada wa kumtimua Ruto serikalini – Kositany

Na SAMMY WAWERU

WANAOANDAA Mswada wa kumtimua Naibu wa Rais Dkt William Ruto serikalini waulete hatuuogopi, amesema mbunge wa Soy Caleb Kositany.

Bw Kositany hata hivyo amesema sheria lazima zifuatwe kabla ya kuuwasilisha bungeni.

“Lazima sheria za kutimua kiongozi aliyechaguliwa na umma zifuatwe kikamilifu,” akasema mbunge huyo.

Baadhi ya viongozi na wanasiasa wanaohusishwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga chini ya vuguvugu la Kieleweke wamekuwa wakitishia kumtimua Dkt Ruto serikalini kwa kile wanahoji “ni kutomheshimu Rais kwa kuanza kampeni za mapema kuchaguliwa 2022”.

Katika mikutano kadha ya umma, Naibu wa Rais amenukuliwa akidai kuna njama ya kumuondoa kutoka wadhifa wake.

Kulingana na Bw Kositany, kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa, mikakati ifaayo kisheria na Kikatiba inapaswa kufuatwa.

“Nahimiza watu wasiogope, kama vile hatukuogopa mswada wa kumfurusha Bw Mike Sonko,” mbunge huyo akasema.

Desemba 2020, Bw Sonko alivuliwa wadhifa wa ugavana Nairobi na madiwani kwa tuhuma za ufisadi, ufujaji na matumizi mabaya ya umma ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi.

Uamuzi wa madiwani wa Kaunti ya Nairobi ulitiwa muhuri na bunge la seneti.

Kifungu cha 150 cha Katiba ya Kenya kimeeleza bayana kuhusu kuondolewa mamlakani kwa naibu wa Rais.

Sheria zilizoorodheshwa kwenye Kifungu cha 144, kumtimua Rais, ndizo zinapaswa kufuatwa kumuondoa naibu wake madarakani.

You can share this post!

Kositany asema ataishtaki Jubilee kwa kumtimua

Hit Squad kushiriki mashindano ya masumbwi DRC