• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
JAMVI: Huenda corona ikamnyima Uhuru usemi 2022

JAMVI: Huenda corona ikamnyima Uhuru usemi 2022

Na CHARLES WASONGA

MIKAKATI ya kupambana na kuenea kwa virusi hatari vya Corona na hatua alizotangaza Rais Uhuru Kenyatta kupunguza athari za janga hili kwa uchumi yamkini hazimfaidi ‘wanjiku’.

Kulingana na wachanganuzi, maagizo hayo yaliyowekwa na serikali kuzuia kuenea kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo yameonekana kuwaumiza wananchi hao wa kawaida zaidi.

Vile vile, afueni ya ushuru ambayo Rais Kenyatta alitangaza Jumatano imeonekana kufaidi asilimia chache ya wale walioajiriwa na kampuni kubwa huku ikiwaacha nje Wakenya wanaochuma mapato katika sekta ya Jua Kali.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) 2018 inaonyesha kuwa, jumla ya watu 14.9 milioni hutegemea sekta hii, inayojumuisha wafanyabiashara wa mapato madogo.

Japo, inakubalika kuwa janga hili halikutarajiwa kutokea, wadau katika sekta zilizoathirika kama vile matatu, wanahisi kwamba Rais Kenyatta angeamuru bei ya mafuta ipunguzwe ili kuwakimu kutokana na hasara ya kupunguza idadi ya abiria.

Hii ndio maana kulingana na mchanganuzi wa masuala ya uongozi na siasa Barasa Nyukuri, watu wanaotegemea sekta hiyo wanakerwa na jinsi Rais Kenyatta anavyoshughulikia janga hilo.’

Rais alipasa kuondoa kabisa ushuru wa thamani (VAT) wa Sh8 kwa lita ya mafuta ulioanza kutozwa mwaka jana ili kuwafaidi wahudumu katika sekta ya uchukuzi ambao wameathirika na amri ya kupunguzwa kwa idadi ya abiria,’ anasema.

‘Na hali itakuwa mbaya kuanzia Ijumaa serikali itakapoanza kutekeleza kafyu aliyoitangaza Rais Jumatano,’ asema Bw Nyukuri.

Kulingana na mchanganuzi huyu, hatua ya Rais kuondoa ushuru wote unaotozwa wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya Sh24,000 na kupunguza ushuru wa mapato (PAYE) kwa wafanyakazi wengine kutokana asilimia 30 hadi 25 inafaidi idadi ndogo ya Wakenya.

‘Kupunguzwa huku kwa ushuru hakuna manufaa yoyote kwa Wakenya ambao tayari wamefutwa kazi katika sekta za utalii, maua na uchukuzi. Na wale waliokuwa wakifanyakazi katika baa, vilabu vya burudani na masoko pia wamepoteza ajira,’ Bw Nyukuri anaongeza.

Katika hali hii, kuna dhana inayojitokeza kwa huenda Rais Kenyatta akaonekana machoni mwa Wakenya wengi kama kiongozi ambaye hakutumia mamlaka yake kuwakinga kika milifu dhidi athari za janga la corona.

Hii, wadadisi wanasema, itaathiri ushawishi wake na haswa uwezo wake wa kuelekeza siasa za urithi na mageuzi ambayo anapania kufanikisha kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Isitoshe, kwa mujibu wa Bw Martin Andati, hatua ya Naibu Rais kuonekana kujiweka pembeni, au kutengwa, katika mchakato mzima wa kukabilina na janga la Covid- 19 imemwacha Rais Kenyatta kuelekezewa lawama zote zinazotokana na mpango huo.

‘Mkurupuko huo wa virusi vya corona, athari zake kwa uchumi Kenya na mikakati ambayo serikali imeweka kudhibiti kusambaa kwake na kuwasadia Wakenya, ni mtihani mkubwa kwa Rais Kenyatta. Bila shaka ina athari nyingi kwake kisiasa wakati huu anajiandaa kuondoka afisini baada ya miaka miwili,’ anasema.

Kulingana na Bw Andati, kando na lawama za hapa na pale kuhusu mikakati aliyoweka kukabiliana athari za janga hili, mkurupuko huu umezima mirindimo ya BBI.

‘Ni wazi kwamba Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walikuwa wakitumia mchakato wa BBI kuunda miungano mipya ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Mipango hii sasa imesitishwa kwa muda na virusi vya corona,’ anasema.

Mipango hii ilitarajia kufanikishwa kupitia mageuzi ya katiba na bila shaka ingemfaidi Rais Kenyatta. Hii ni kwa sababu baadhi ya wandani wake walianza kupendekeza atengewe wadhifa wa Waziri Mkuu.

Baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kugunduliwa nchini, serikali ilipiga marufuku mikutano yote ya hadhara nchini.

Hatua hiyo iliathiri mkutano wa BBI ambao ulipangwa kufanyika katika uwanja wa Afraha, Nakuru, mnamo Machi 21.Kabla ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza hatua hiyo, Rais Kenyatta alikuwa amekutana na magavana 11 kutoka Kaunti za Rift Valley kuarifiwa kuhusu maandalizi ya mkutano huo.

Na Bw Andati anasema hatua ya Dkt Ruto ya kutohudhuria vikao vingi vya kujadili mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo pia imetoa taswira ya kutokuwepo kwa mshikamano serikalini.

‘Wiki jana, Naibu Rais alikosa kuhudhuria mkutano wa Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC), ishara kwamba uhusiano wake na bosi wake bado sio mzuri hata wakati huu ambapo Wakenya wanatarajia mshikamano mkubwa serikalini,’ anaeleza.

Dkt Ruto pia hajaandamana na Rais anapohutubia taifa kutangaza hatua mbalimbali ambazo serikali imechukua kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona katika jumba la Harambee, Nairobi.

You can share this post!

KAFYU: Msongamano Likoni wapunguzwa

CORONA: Kimya makanisani, waumini wakimbilia YouTube

adminleo