• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Kavindu aapishwa rasmi kuwa Seneta wa Machakos

Kavindu aapishwa rasmi kuwa Seneta wa Machakos

Na CHARLES WASONGA

BI Agnes Kavindu Muthama, Jumanne aliapishwa rasmi kuwa Seneta wa Machakos katika hafla fupi iliyoongozwa na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.

Shughuli hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Seneti, Nairobi pia ilishuhudiwa na kiongozi wa Wiper Stephen Kalonzo Musyoka.

Bi Kavindu aliibuka mshindi wa kiti hicho katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi wiki jana.

Alimshinda mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), ambaye ndiye alikuwa mpinzani wake wa karibu.

Bi Kavindu alizoa jumla ya kura 104,354 na kumshinda kwa umbali zaidi Bw Ngengele aliyepata kura 19,726 pekee.

Seneta huyo mpya wa Machakos alisindikizwa kuingia ndani ya ukumbi wa Seneti na kiongozi wa Ford Kenya ambaye pia ni Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula na seneta maalum Abshiro Halakhe.

Bw Wetang’ula ni mmoja wa vigogo wakuu katika muungano wa “One Kenya” unaoshirikisha Bw Musyoka, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na Mwenyekiti wa Kanu na Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Kando na Bw Musyoka, sherehe hiyo ya kumwapisha Bi Kavindu pia ilihudhuriwa na Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Wavinya Ndeti, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki.

Pia walikuwepo wabunge; Julius Mawathe (Embakasi Kusini), Stephen Mule (Matungulu), Edith Nyenze (Kitui Magharibi), Robert Mbui (Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kathiani) na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Machakos katika Bunge Bi Joyce Kamene.

Bi Kavindu achukua nafasi ya Boniface Kabaka aliyefariki mnamo Desemba 15, 2020, kutokana na ugonjwa wa moyo. Seneta huyo mpya ni mwanamke wa nne kuchaguliwa kama Seneta chini ya Katiba ya sasa iliyozinduliwa mnamo 2010.

Wengine ni; Fatuma Dullo (Isiolo), Susan Kihika (Nakuru) na Prof Margaret Kamar (Uasin Gishu) ambao wote walichaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2017.

You can share this post!

Kipa Sergio Romero kuagana rasmi na Man-United mwishoni mwa...

Wageni kutoka Tanzania kuwekwa karantini Mombasa