• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Rufaa ya BBI kung’oa nanga juma lijalo

Rufaa ya BBI kung’oa nanga juma lijalo

MAHAKAMA ya Rufaa imeamuru kesi ya kupinga mchakato wa mageuzi ya Katiba (kupitia mswada wa BBI) isikizwe Juni 2, 2021.

Rais wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Daniel Musinga aliamuru mawakili wa kinara wa ODM Raila Odinga, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Mwanasheria Mkuu waliokata rufaa hiyo wafike kortini.

Wengine watakaofika mahakamani ni pamoja na walalamishi waliowasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu, miongoni mwao mtaalam wa masuala ya kiuchumi, Dkt David Ndii.

Jaji Musinga aliamuru wahusika wote wafike mbele ya majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kuwasilisha tetezi zao na kupata mwelekeo zaidi kuhusu jinsi ya kusikiza rufaa zilizowasilishwa kwa lengo la kurejelea mchakato wa BBI kabla ya kura ya maoni kupigwa.

Jaji Musinga alisema mahakama itatoa mwelekeo iwapo rufaa kamili itasikizwa ama ni maombi ya kuzima kusikilizwa kwa kesi hiyo yatakayosikilizwa.

Mawakili Mutuma Gichuru, Nelson Havi na Morara Omoke waliandikia mahakama ya rufaa wakiomba kesi hiyo isikizwe na ama majaji saba au 11.

“Rufaa zilizowasilishwa zitasikizwa Juni 2, 2021 kutoa mwelekeo iwapo maombi yaliyowasilishwa yatasikizwa kwanza ama rufaa kamili itaanza kusikizwa moja kwa moja,” msajili wa mahakama ya rufaa, Bw Moses Serem alisema katika arifa aliyopelekea mawakili wanaohusika.

Katika rufaa iliyowasilishwa na mwanasheria mkuu aliye pia mshauri wa serikali, Bw Kihara Kariuki, mahakama inaombwa ifutilie mbali uamuzi huo wa majaji watano wa mahakama kuu waliosema sheria na katiba hazikufuatwa pale mchakato wa BBI ulipozinduliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Majaji hao watano walisema kuwa kifungu cha 232 cha katiba hakikufuatwa katika mchakato wa kuifanyia mageuzi.

Pia majaji hao walisema Rais Kenyatta alivunja sheria alipojitosa katika harakati ya kugeuza katiba ilhali kazi hiyo ni ya bunge au wananchi wa kawaida.

Bw Kihara anasema endapo rufaa hiyo haitaamuliwa upesi basi huenda Rais Kenyatta akashtakiwa kwa kukaidi na kukiuka Katiba.

Mahakama hiyo inaombwa ifutilie mbali uamuzi huo wa majaji watano kwa kupiga breki mchakato huo unaathiri maslahi ya umma ikitiliwa maanani mabilioni ya pesa yalitumika kuufikisha kiwango cha sasa.

You can share this post!

Walimu hatarini kukosa nyongeza ya mishahara

Ruto kuteua mwaniaji mwenza bila kushauri viongozi wa UDA