• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Tuju sasa awataka wanachama waasi wahame Jubilee

Tuju sasa awataka wanachama waasi wahame Jubilee

Na WANDERI KAMAU

KATIBU Mkuu wa Chama cha Jubilee (JP), Bw Raphael Tuju, amesema kuwa viongozi wa ‘Tangatanga’ waliobaki katika chama hicho wako huru kuondoka badala ya kuendelea kulalamika.

Bw Tuju alisema kuwa haina maana kwa viongozi hao kuendelea “kupiga kelele” wakiwa bado ndani ya chama ambacho hawana imani na uongozi wake.

Mrengo huo umejitokeza kupinga vikali mpango wa Jubilee kubuni muungano wa kisiasa na chama cha ODM, ukitaja hatua hiyo kama “usaliti.”

Wikendi iliyopita, Naibu Rais William Ruto alikitaja chama cha UDA kama “mpango mbadala” wa mrengo huo ikiwa Jubilee itaungana na ODM.

Lakini kwenye mahojiano, Bw Tuju aliwafananisha viongozi hao na “mwanamke aliyechoshwa na ndoa.”

Alisema ni kinaya kwa wanasiasa hao kulalamikia hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kupanua juhudi za kuleta amani na uthabiti wa kisiasa nchini, ilhali juhudi kama hizo ndizo zilibuni muungano kati ya Rais na Dkt Ruto mnamo 2012.

“Rais ameamua kuwafikia viongozi wengine ili kuleta umoja kamili nchini. Sababu kuu ni kuwa handisheki ya kwanza kati yake na Dkt Ruto ilizishirikisha jamii za Wakikuyu na Wakalenjin pekee,” akasema Bw Tuju.

Akihutubu wiki iliyopita, Dkt Ruto aliwarai Wakenya kutokubali kuingizwa kwenye “mtego wa NASA” tena.

Wanasiasa katika mrengo huo wamekuwa wakiwalaumu viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Bw Tuju, Naibu Mwenyekiti David Murathe, Mbunge Maalum Maina Kamanda kati ya wengine kwa “kukiteka chama” na kufanya uamuzi wa kuwafurusha bila kuzingatia taratibu zifaazo.

Wabunge waasi walijipata pabaya baada ya kufurushwa kutoka kamati mbalimbali za Bunge la Kitaifa kama “adhabu” ya kujihusisha na Dkt Ruto na kukaidi agizo la Rais Kenyatta kutoendeleza kampeni za 2022.

Mrengo huo umekuwa ukiwalaumu viongozi hao kwa “kumpotosha” Rais Kenyatta kuhusu uthabiti wa chama na masuala yanayowaathiri Wakenya.

Kwenye mahojioano na runinga moja majuzi, Dkt Ruto alitaja Jubilee kuwa “chama kilichovurugika baada ya kutekwa nyara na viongozi wachache wabinafsi.”

“Huwa tunashangazwa na baadhi ya uamuzi tunaoshuhudia. Kwa mfano, hakujakuwa na mkutano wowote wa chama kujadili kuhusu muungano wa kisiasa na ODM. Hili ndilo limezua uasi uliopo,” akasema Dkt Ruto.

Wanasiasa hao wameapa kuonyesha Jubilee kivumbi kwenye uchaguzi mdogo wa eneo la Kiambaa, Kaunti ya Kiambu, unaotarajiwa kufanyika Julai 15.

Jubilee imemsimamisha mwanasiasa Kariri Njama huku UDA ikimpigia debe John Njuguna, almaarufu “Ka Wanjiku.”

  • Tags

You can share this post!

Khan ajiondoa katika kesi ya Gicheru ICC

Wembe wenye jina linalokaribiana na al-Shabaab wapigwa...