• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Wandayi akana muungano kati ya Raila na Ruto

Wandayi akana muungano kati ya Raila na Ruto

Na RUSHDIE OUDIA

CHAMA cha ODM, chake waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, hakina mipango ya kubuni muungano na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya kisiasa katika chama hicho alisema badala yake chama hicho kitaendelea kusukuma kufanyika kwa kura ya maamuzi kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Vile vile, alisema chama hicho kitaendeleza ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta kupitia handisheki.Bw Wandayi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu wa Fedha za Umma (PAC) alisema kile kinachoendelea nchini kwa sasa na hali ya wanasiasa kujitakia makuu kisiasa na “hatutishwi hata kidogo.”

Aliongeza uchaguzi mkuu ujao unapokaribia, wanasiasa wataendelea kujipanga kwa kubuni miungano ili waweze kuboresha nafasi zao za kushinda.

“Kile kinachoendelea ni hali ya kawaida ya wanasiasa kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 kwa kujaribu kubuni miungano. Suala la ODM kuungana na UDA haliko mezani sasa. Wakati huu tunaangazia BBI na huko ndiko tunakoelekeza juhudi zetu zote,” akasema Bw Wandayi.

Alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Bw Odinga kuorodheshwa miongoni mwa viongozi watatu wa chama hicho watakaowania nafasi ya kupeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Wengine, waliowasilisha barua zao za maombi na kulipa Sh1 milioni iliyohitajika ni manaibu wa Bw Odinga chamani; Wycliff Oparanya na Ali Hassan Joho ambao ni magavana wa Kakamega na Mombasa, mtawalia.

Awali, kakake Bw Odinga, Oburu Odinga alidokeza kuhusu uwezekano wa kiongozi huyo wa ODM na Dkt Ruto kuungana ili waweze kukabilaina na muungano wa One Kenya Alliance.

Muungano huo unawaleta pamoja kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenyekiti wa KANU Gideon Moi.Wiki moja iliyopita, Naibu Rais pia alidokeza kuhusu uwezekano wake kufanya kazi na Bw Odinga.

Dkt Ruto aliwahi kuwa mwanachama wa jopo la Pentagon katika chama cha ODM kabla ya uchaguzi mkuu wa 2007.Akihojiwa na Redio Citizen Dkt Ruto alisema kuwa tofauti kati yake na Bw Odinga na ya kisiasa wala sio ya kibinafsi na kwamba wote wawili wanaamini katika uundaji wa chama cha kitaifa kitakachowaleta Wakenya wote pamoja wala sio vyama vya kikabila.

Eliud Owalo ambaye ni mwandani wa Naibu Rais kutoka Luo Nyanza alisema ni mapema zaidi kuzungumzia muungano wowote kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto.Tayari vijana wa chama cha UDA, tawi la Kisumu wameanza kupatwa na msisimko huku wakionyesha urafiki na wenzao wa ODM.

You can share this post!

Polisi ahepa kazi Mombasa kufukuzia penzi la mama...

UHURU AMTULIZA RAILA