• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Sudan Kusini yakashifiwa kwa ‘kusambaza’ chanjo ya corona

Sudan Kusini yakashifiwa kwa ‘kusambaza’ chanjo ya corona

JUBA, Sudan Kusini

Na DAVID MAYEN

WADAU katika mchakato wa kudhibiti msambao wa Covid-19 nchini Sudan Kusini wamekashifu hatua ya serikali ya nchi hiyo kutoa dozi 72,000 za chanjo kwa nchi jirani baada ya kushindwa kuzisambaza nchini humo.

Wiki hii, mamlaka jijini Juba iliamua kuipa Kenya dozi hizo za chanjo ya AstraZeneca, kupitia mpango wa usambazaji chanjo wa COVAX, kwa kuhofia kuwa muda wao wa matumizi utapita chini ya utaratibu wa sasa wa utoaji chanjo.

Sudan Kusini imeshindwa kutoa chanjo hiyo kwa haraka kwani imefaulu kutoa dozi zisizozidi 20,000 ndani ya kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja.

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanasema kurejeshwa kwa dozi hizo ndio hatua bora kwa serikali hiyo ambayo imeshindwa kutumia mitandao bora kutoa chanjo ya Covid-19.

Mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Foundation for Democracy and Accountable Governance James Kolok alisema imekuwa vigumu kwa serikali ya Sudan Kusini kusambaza chanjo ya Covid-19 kwa sababu umma haujapewa uhamasisho wa kutosha.

“Hali hii inaiweka Sudan Kusini katika hatari zaidi ikizingatiwa kuwa aina mpya za virusi vya corona imegunduliwa katika taifa jirani la Uganda. Kimsingi, serikali ilifanya kosa kubwa kwa kurejesha chanjo,” akasema,

Bw Kolok akaongeza : “Sharti serikali iwachanje watu. Kurejesha chanjo kutatoa taswira mbaya kwamba watu hawahitaji kupewa chanjo ya kuwakinga dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona”

Sudan Kusini ilipokea dozi 132,000 za chanjo wa AstraZeneca mapema mwezi Machi chini ya mpango wa usambazaji chanjo kwa mataifa yenye uwezo finyu kifedha, COVAX.

Vile vile, ilipokea dozi nyingine 60,000 kutoka wa Umoja wa Afrika (AU). Lakini usambazaji wa chanjo hiyo pole pole umelazimisha mamlaka kusitisha shughuli hiyo baada ya muda wa matumizi wa nyingi za dozi kupita.

Awali, Sudan Kusini ilitarajiwa kupokea shehena kadha za chanjo chini ya mpango wa COVAX huku Wizara ya Afya ikipanga kutoa chanjo hiyo kwa angalau asilimia 40 ya idadi jumla ya watu nchini humo ifikapo mwaka wa 2022.

Hata hivyo, kufikia Mei 24, ni dozi 16,000 ambazo zilikuwa zimesambazwa, zote katika jiji la Juba pekee.

Dkt Anthony Garang, kiongozi wa Chama cha Madaktari Nchini Sudan Kusini naye amedai idadi ndogo ya watu wanaojitokezwa kupokea chanjo ya corona inachangiwa na kuenea kwa habari za kupotosha kuhusu chanjo hiyo ya AstraZeneca.

Dkt Garang ameitaka serikali kuzidisha kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu chanjo hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Wito wazee wa nyumba 10 walipwe kusambaza kadi za Huduma...

TUZO ZA EPL: Beki Ruben Dias na kocha Pep Guardiola waibuka...