• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Sonko atambuliwa kimataifa kwa ‘ukarimu’ wake

Sonko atambuliwa kimataifa kwa ‘ukarimu’ wake

NA CECIL ODONGO

GAVANA wa NairobI Mike Mbuvi Sonko Jumanne alitambuliwa kimataifa na kupokezwa wadhifa wa Balozi wa Shirika la Kimataifa la kijamii la Matendo Mema na serikali ya Israeli kutokana na vitendo vyake vya ukarimu katika jamii.

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo Kaynan Rabinho vile vile alimsifu Bw Sonko kwa kurembesha sehemu ya barabara kuu ya Nairobi- Mombasa iliyoka katika kaunti yake kwa fedha zake mwenyewe.

“Tumekuwa tukitazama kanda ya video zinazoonyesha jinsi ulivyojitolea kusaidi wasiobahatika katika jamii. Wewe ni kiongozi ambaye anafaa kuigwa na wengi. Watu hawafahi kuchukulia ukarimu wako vivi hivi tu kwa sababu kile umefanya kinastahiki na kinatambuliwa ulimwenguni,” akasema Bw Rabinho.

Afisa huyo alikuwa akizungumza alipomtembelea Bw Sonko katika ofisi yake ya City Hall jijini Nairobi.

Kulingana naye, jiji la Nairobi ni hazina kubwa ya uwekezaji wa kibiashara ndiyo maana shirika lake limeamua kushirikiana na gavana huyo kuandaa Kongamano kubwa la Kimataifa la Matendo Mema mwezi Aprili mwakani mjini Nairobi.

Kwa upande wake, Bw Sonko akikubali tuzo hiyo aliuhakikishia ujumbe huo kutoka Israeli kwamba uongozi wake unajituma sana ili kuimarisha maisha ya wakazi wa jiji la Nairobi.

“Nashukuru sana kwa kutajwa kuwa balozi wa Matendo Mema nchini Kenya. Nitaendelea kutenda mema ili kuleta usawa miongoni mwa raia wote na kuhakikisha kwamba shirika hili linaandaa kongamano kubwa la kufana mwakani,” akasema Bw Sonko.

Afisa Mkuu wa Shirika la Kimataifa la SBI Holdings Denis Repushinski pia alihudhuria kikao cha jana.

You can share this post!

ONYANGO: Nia ya kufadhili vyama hivi vya kisiasa haifai

Ubugiaji pombe husaidia kuzungumza lugha za kigeni kwa...

adminleo