• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Tupatane mahakamani, Dorcas Mwende amwambia mamaye Jackline Nzilani

Tupatane mahakamani, Dorcas Mwende amwambia mamaye Jackline Nzilani

COLLINS OMULO NA WANGU KANURI

Dorcas Mwende hana majuto. Isitoshe, yupo tayari kwa hukumu itakayothibitisha ukweli kuhusu madai aliyomsingizia babake, Julius Wambua kuanza.

Binti huyu mwenye umri wa miaka 24 anasubiri kwa hamu kumuona mamaye, Jackline Nzilani kortini ili wingu hili jeusi la kujuta lililotanda maishani mwake liweze kuondoka. Kwake Mwende, kufungwa kwa babake kulimfanya mtumwa kifikra na kesi hii ikiisha haraka itamsaidia.

“Wacha alete madai aliyonayo kortini. Niko tayari kuonana naye ana kwa ana. Sitaki kuzungumza mengi kuhusu jambo hili. Anajua siku ya kwenda kortini. Wacha tupatane ana kwa ana huko mahakamani,” akaambia Taifa Leo Dijitali kwa njia ya simu.

Hata ingawa alikataa ombi la mahojiano ya moja kwa moja, anasema hakuna haja kuanika familia yake kwa umma haswa kwa kuwa inamhusu mamake.

Lakini swali ambalo bado Mwende anajiuliza ni mbona mamake alinyamaza kwa muda mrefu hivyo.

“Kutoka siku ile nilivumbua niliyosema, mbona hakuja kupinga niliyosema wakati huo? Je, sasa ndivyo amejua nilikuwa nadanganya? Kutoka 2015 alijua nilikuwa na mtazamo tofauti wa mambo. Angekuja wakati huo aseme maoni yake kuhusu niliyosema,” asema mzaliwa huyo wa pili.

Wakati ambapo majuto ya kumsingizia babake kwa kutoa ushahidi usio wa kweli haukumpa amani akilini, aliamua kuenda jela ya Kamiti kukiri yote yaliyofanyika kwa babake.

“Ukiwakosea wazazi wako, kuna hisia ya majuto inayokufanya uombe msamaha. Majuto moyoni mwangu yalinifanya kuchukua hatua ya kwanza kwa kumtembelea babangu. Huo ulikuwa mwaka wa 2015 na nikakiri yote kupitia afisa aliyekuwa zamu, jelani hiyo ya Kamiti,” Mwende anaongezea.

Yuko tayari kufurahia amani ijayo baada yake kuungama. Kwa sababu hii, anahamu ya maendeleo ya korti na anatumai kesi hii iweze kuisha.

“Hakuna vile ukweli utafunganywa na uongo. Mungu ndiye ukweli na hakuna vile ukweli unaweza badilishwa na kuwa uongo. Unaweza uficha ukweli lakini utajulikana mwishowe,” akasema Mwende.

Msukosuko huu ulioanza mwaka wa 2008 sasa unatishia kugawanya familia hata zaidi huku binti na mamake wakiwa kwenye ‘kinyanganyiro.’

Ripoti ya daktari kutoka kituo cha kliniki ya Medecins Sans Frontieres Blue House Recovery iliyoonwa na Taifa Leo Dijitali inaonyesha kuwa Mwende hakuwa na majeraha yoyote ya kimwili.

Sehemu zake za siri zilikuwa sawa lakini uwazi wa uke wake ulikuwa umepanuka huku ukitoa umajimaji unaonuka wa rangi nyeupe. Pia ubikira wake ulikuwa umevunjika. Ripoti hiyo inasema kuwa wakati wa mashauriano, Mwende alisema kuwa alidhulumiwa kingono na babake mara nyingi kutoka mwezi wa Machi na Aprili 2011.

Ni ripoti ambayo korti ya Kithimani kupitia hakimu mkuu AW Mwangi ilitumia pamoja na ushahidi kutoka Mwende na dadake mdogo, Anastacia Mukulu iliyomhukumu BwWambua kwa kifungo cha maisha jelani.

Lakini Mwende anasema kuwa mamake alimshauri kumsingizia babake ili aweze kuipata shamba la familia na pia amfukuze mke wa pili aliyeletwa na Bw Wambua pindi tu walipoachana.

“Hakuwa na furaha kuhusu mke huyo wa pili na akatumia hila ya kunifanya nimsingizie babangu ili amfukuze mke huyu wa pili na aweze kuiuza shamba la familia wakati ambapo babangu amefungwa gerezani. Hakufaulu,” asema Mwende.

Hata hivyo, mamake Mwende, Bi Nzilani anayakataa madai hayo dhidi ya mke wa pili, ambaye anasema walikuwa na uhusiano na bwanake kabla hawajaoana. Pia anayakataa madai kuwa alitaka kuuza shamba kama inavyoelezwa.

Bw Wambua kwa upande wa pili anasema kuwa hana kinyongo chochote kwa mkewe.

Anasema kuwa alishamsamehe na yuko tayari kupatana na Bi Nzilani. Hata hivyo, mkewe amesema hana chochote cha kufanya naye na hana chochote cha kuombea msamaha.

You can share this post!

2020: Corona ilivyozamisha sekta ya elimu

Muthama na Koech wataka walipwe fidia baada ya kukamatwa