• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Viongozi wataka Mvurya avalie joho la Sultan

Viongozi wataka Mvurya avalie joho la Sultan

VALENTINE OBARA na BRIAN OCHARO

GAVANA wa Kwale, Bw Salim Mvurya, ametiwa presha ajitokeze wazi kuubeba mwenge wa kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa Wapwani.

Gavana huyo ambaye ni nadra kuonekana akipiga siasa wakati usiofaa, amejizolea sifa tele baada ya kuongoza kampeni za Feisal Bader ambaye aliibuka mshindi wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Msambweni uliofanyika Desemba 15.

Bw Bader aliyepata kura 15,251 alimshinda mwaniaji wa chama cha ODM, Bw Omar Boga ambaye alikuwa ametabiriwa na wadadisi wengi kushinda kiti hicho. Bw Boga alipata kura 10,444.

Waliotabiri hayo walizingatia umaarufu wa ODM katika maeneo mengi ya Pwani na umaarufu wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho aliye pia Naibu Kiongozi wa chama hicho.

Jana, Naibu Rais William Ruto aliongoza hafla katika Kaunti ya Kwale kusherehekea ushindi wa Bw Bader.

Viongozi wengi waliohutubu walimtaka Bw Mvurya sasa achukue rasmi jukumu la kutolea Wapwani mwelekeo wa kisiasa, jukumu ambalo kwa muda mrefu limeonekana kuwa mikononi mwa Bw Joho aliye maarufu kama ‘Sultan’.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, alisema matokeo ya uchaguzi mdogo Msambweni yanafaa kutumiwa na Wapwani kama mwanzo mpya wa kujikomboa kutoka kwa minyororo ya vyama ambavyo, kulingana naye, hutolea jamii za ukanda huo ahadi za uongo kila wakati wa uchaguzi.

Bi Jumwa alitoa wito kwa Wapwani waungane kutimiza azimio la kuwa na chama kimoja kitakachotetea maslahi yao, na wamruhusu Bw Mvurya kushika usukani wa chama hicho.

“Mvurya nataka utukubalie sisi wakazi wa Pwani tukupeleke katika meza ya kitaifa inayofanya maamuzi, ili Mpwani apate kuwa na sauti mpya. Tulichojua ni kuwa Joho hakuwa na mpango wowote isipokuwa majigambo na majivuno,” akasema.

Wito sawa na huu ulitolewa na viongozi wengi ambao walihutubia umati katika hafla hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Babla, Ukunda.

Aliyekuwa Seneta wa Taita Taveta, Bw Dan Mwazo, alisema ushindi wa Bw Bader ulithibitisha uwezo wa Bw Mvurya ‘kukomboa Wapwani’.

“Umeonyesha mfano mzuri kukomboa Wapwani. Wewe Pwani ni nambari moja. Nimejitolea kukuzungusha Taita Taveta, Tana River na kila mahali ili tukomboe Wapwani,” akasema.

Katika hotuba yake, Bw Mvurya alisema wimbi la mageuzi kwa Wapwani limeanzia Kwale kwa hivyo wanasiasa watambue hakuna nafasi ya kuhadaa wakazi tena.

Alikashifu wapinzani wa Bw Bader kwa kutumia matusi katika kampeni zao badala ya kueleza wananchi sera walizokuwa nazo.

“Hapa hakuna nafasi ya siasa za kudanganyana wala utapeli. Hawa Wakwale na Pwani nzima kwa jumla wanahitaji kusaidiwa mambo ya elimu, afya na uchumi. Hawahitaji uongozi wa kukuza jina la mtu mmoja. Nawaambia bila malipo kwamba itakuwa vigumu kubadilisha akili za watu waliozinduka,” akasema gavana.

Viongozi wengine waliokuwepo katika hafla hiyo ni Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, Gavana wa Turkana Josphat Nanok miongoni mwa wengine.

Mnamo Jumanne, Bw Odinga alikutana na viongozi wa chama chake Kwale kutathmini sababu zilizowasababishwa kushindwa katika uchaguzi huo.

Gavana Joho awali alisema matokeo ya uchaguzi huo mdogo hayafai kutumiwa kupima umaarufu wa chama wala kiongozi kwa vile wapigakura walioshiriki walikuwa wachache mno.

You can share this post!

Wanafunzi wa wazazi wasio na karo wasifukuzwe shuleni...

Pwani walisota zaidi Kenya 2020 – Utafiti